WABUNGE EALA WAANZA KUJADILI BAJETI YA EAC, MASUALA YA MIPAKANI YAPEWA KIPAUMBELE
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) limeanza rasmi kikao chake cha bajeti jijini Arusha, ambapo wabunge kutoka nchi wanachama wanatarajiwa kujadili na kuidhinisha Bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa mwaka wa fedha 2026/2027 pamoja na masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano na maendeleo ya kikanda.
Kabla ya kuanza kwa mijadala ya bunge, kamati mbalimbali za EALA zilifanya vikao vyao na kuwasilisha ripoti ambazo zimeanza kujadiliwa katika kikao hicho cha bajeti. Miongoni mwa agenda kuu ni kupitia matumizi ya taasisi za jumuiya na kuweka vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli za EAC kwa mwaka ujao wa fedha.
Kikao hicho kinahusisha pia kujadili na kuidhinisha bajeti za taasisi mbalimbali za jumuiya ikiwemo Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), Sekretarieti ya EAC pamoja na taasisi nyingine zilizo chini ya mwavuli wa jumuiya hiyo.
Katika siku ya kwanza ya kikao hicho, wabunge walijadili ripoti ya Kamati ya Hesabu za Fedha, ambayo ilijikita katika tathmini ya matumizi na usimamizi wa rasilimali za jumuiya. Wajumbe walisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha ili kuhakikisha taasisi za EAC zinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wakati huo huo, Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Utalii iliwasilisha taarifa yake iliyojadili changamoto zinazokabili maeneo ya mipakani kati ya nchi wanachama. Wabunge walieleza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyochelewesha usafirishaji wa watu na bidhaa katika mipaka ya Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine za jumuiya.
Kamati hiyo ilitoa mapendekezo mbalimbali yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara ya kikanda, kuongeza ufanisi wa huduma za mipakani na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii miongoni mwa nchi wanachama.
Akizungumza jijini Arusha, Mbunge wa EALA, Machano Ali Machano, amesema ana matumaini makubwa kuwa kikao hicho kitazaa maamuzi yatakayochochea maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuimarisha utekelezaji wa malengo ya ushirikiano wa kikanda.
"Wabunge wanaendelea kutekeleza majukumu yao katika mazingira mazuri ya kazi, na tunaamini mijadala ya bajeti hii itasaidia kuimarisha taasisi za jumuiya na kuleta manufaa kwa wananchi wa Afrika Mashariki," amesema.
Wabunge wa EALA wanatarajiwa kupitisha Bajeti ya EAC ya mwaka wa fedha 2026/2027 katika siku zijazo, hatua itakayoweka msingi wa utekelezaji wa mipango na shughuli za jumuiya kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.
Ends


Post a Comment