Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameiagiza kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 70 katika Jiji la Arusha kwa kufanya kazi mchana na usiku, huku Serikali ikisisitiza kuwa kilomita 13 za mradi huo zenye umuhimu kwa maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 lazima zikamilike kabla ya Januari mwaka 2027.
Akizungumza na wananchi wa Kiseriani na Kwa Mrombo, Waziri Ulega alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutoa kipaumbele kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ili kuboresha maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa taifa.
Alieleza kuwa mradi huo wa kilomita 70 ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mtandao wa barabara ndani ya Jiji la Arusha, ukiunganisha maeneo mbalimbali muhimu ikiwemo , Mbauda, Kwa Mrombo, Barabara ya Bypass, Soko la Kilombero hadi Uwanja wa Ndege wa Kisongo hadi AFCONI
Waziri huyo aliagiza mkandarasi kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati mmoja katika maeneo yote ya mradi kwa kuweka kambi zinazojitegemea zenye mitambo, wataalamu na wafanyakazi wake ili kuondoa ucheleweshaji unaotokana na kuhamisha vifaa kutoka eneo moja kwenda jingine.
"Nataka kila sehemu ya mradi iwe na vifaa vyake, wataalamu wake na wafanyakazi wake. Kazi zifanyike kwa wakati mmoja katika maeneo yote. Ongezeni mitambo, ongezeni wafanyakazi na hakikisheni mnafanya kazi mchana na usiku ili mradi ukamilike kwa wakati," alisisitiza.
Aidha, alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia kazi zisizo na ubora, akieleza kuwa fedha zinazotumika ni za walipa kodi na hivyo wananchi wanastahili kupata barabara za kudumu na zenye viwango vya juu.
"Hizi ni fedha za walipa kodi. Tunataka barabara zinazodumu na zinazokidhi viwango vya kitaifa.
Hakutakuwa na nafasi ya kufanya kazi chini ya kiwango," alisema.
Pia aliwataka wakandarasi kutoa kipaumbele kwa ajira kwa vijana wa Arusha ili mradi huo uweze kuwanufaisha wananchi kupitia ongezeko la kipato na shughuli za kiuchumi.
Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Reginald Masawe, alisema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 221 unahusisha ujenzi wa kilomita 70, zikiwemo kilomita 55 katika Mkoa wa Arusha na kilomita 15 katika Mkoa wa Manyara.
Alisema mkataba wa mradi ulianza kutekelezwa rasmi Aprili 10, 2026 baada ya mkandarasi kulipwa malipo ya awali na kupewa kibali cha kuanza kazi, huku ukitarajiwa kukamilika Machi 25, 2029.
Hata hivyo, alisema Serikali imeelekeza nguvu kubwa katika ujenzi wa kilomita 13 zinazohusiana na maandalizi ya AFCON 2027, ambazo zinapaswa kukamilika kabla ya Januari mwakani ili kuwezesha ukaguzi wa miundombinu na maandalizi ya mashindano hayo.
"Mkazo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kilomita 13 zinazohusiana na maandalizi ya AFCON zinakamilika kabla ya Januari 2027," alisema Mhandisi Masawe.
Alifafanua kuwa barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha kisasa ikiwa na njia za watembea kwa miguu, mifereji ya kisasa ya maji, taa za barabarani katika maeneo muhimu pamoja na miundombinu mingine itakayoboresha usalama na kuondoa tatizo la mafuriko, hususan katika maeneo ya Mbauda na Kwa Morombo.
Kwa sasa, alisema mkandarasi ameanza kazi za kusafisha eneo la mradi (site clearance), huku utekelezaji ukiwa umefikia takribani asilimia tano na zoezi la kuhamasisha mitambo na vifaa vya ujenzi likiendelea.
Aidha, alisema usanifu wa mradi umekamilika na TANROADS inaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo TANESCO na AUWSA katika kuhamisha miundombinu itakayopisha ujenzi wa barabara.
Alitaja changamoto zinazoweza kujitokeza kuwa ni mvua pamoja na uhamishaji wa baadhi ya huduma za miundombinu, lakini akasisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha hazikwamishi utekelezaji wa mradi.
Ends..










Post a Comment