TIGF KUVUTIA ZAIDI YA DOLA BILIONI 6.5 KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI, SERIKALI YAIPONGEZA KWA KUCHOCHEA DIRA YA 2050
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
SERIKALI imeeleza matumaini makubwa kuwa Mfuko wa Uwekezaji na Ukuaji wa Tanzania (TIGF) utakuwa chachu ya kuvutia mabilioni ya dola za Marekani katika miradi ya maendeleo, hatua inayotarajiwa kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kuifanya Tanzania kuwa moja ya vituo vikuu vya uwekezaji barani Afrika.
Kauli hiyo ilitolewa katika Kongamano la Uwekezaji Tanzania lililoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii (ESRF) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), ambapo viongozi wa Serikali, wawekezaji, taasisi za kifedha na waandaaji wa miradi walikutana kujadili fursa za uwekezaji na upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya miradi ya kimkakati.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki, alisema TIGF imeanzishwa kama jukwaa maalumu la kuunganisha miradi ya maendeleo na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili kusaidia upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa yenye tija kwa taifa.
Alisema mfuko huo ni matokeo ya ushirikiano kati ya Serikali, ESRF na UNDP, ukiwa na lengo la kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali pekee na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika kugharamia maendeleo.
“Tunatarajia TIGF kuwa daraja muhimu la kuunganisha miradi ya maendeleo na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Hii itasaidia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuimarisha ukuaji wa uchumi,” alisema Kairuki.
Alibainisha kuwa maandalizi ya awali tayari yamewezesha kutambuliwa kwa miradi 15 yenye uwezo mkubwa wa kuvutia uwekezaji, yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.35.
Kwa mujibu wake, miradi hiyo inahusisha sekta za nishati, uchumi wa buluu, huduma za kifedha, miundombinu, uhifadhi wa mazingira pamoja na sekta nyingine zinazochangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kairuki alisema wawekezaji wa kimataifa tayari wameonesha nia ya kuwekeza katika baadhi ya miradi hiyo, jambo linalodhihirisha kuendelea kuimarika kwa imani ya jumuiya ya kimataifa kwa mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania.
Aidha, alisema mfuko huo utachangia kuimarisha uwekezaji katika maeneo ya kipaumbele ya Serikali ikiwemo mageuzi ya kidijitali, elimu, afya, maji na ukusanyaji wa mapato, huku ukiwezesha upatikanaji wa mitaji kwa masharti nafuu zaidi kutoka taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Chaya, aliipongeza TIGF kwa mchango wake katika kuhamasisha uwekezaji unaolenga kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Dkt. Chaya alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu, hatua ambazo zimeongeza ushindani wa uchumi wa Tanzania na kuvutia wawekezaji zaidi.
Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka malengo makubwa, ikiwemo kuifikisha Tanzania kuwa na uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, kuongeza mchango wa sekta binafsi katika pato la taifa na ajira pamoja na kuinua kipato cha wananchi.
“Mafanikio ya malengo haya hayawezi kupatikana bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi. Sekta binafsi ndiyo injini kuu ya ukuaji wa uchumi na chanzo kikubwa cha ajira nchini,” alisema Dkt. Chaya.
Alisema Serikali imeendelea kuboresha sera, sheria na mifumo ya uwekezaji ili kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi bora zaidi za uwekezaji barani Afrika, huku ikiendelea kuendeleza Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (SEZs) yanayorahisisha upatikanaji wa ardhi, miundombinu na huduma kwa wawekezaji.
Dkt. Chaya alieleza kuwa tayari wawekezaji wameonesha nia ya kuwekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.5 katika miradi ya maendeleo inayohusisha sekta za usafiri, maji, miundombinu na huduma nyingine za kijamii.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Profesa Fatunata Songora Makene, alisema kongamano hilo limeandaliwa kwa lengo la kuunganisha wawekezaji, Serikali na waandaaji wa miradi ili kuharakisha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Profesa Makene alisema kupitia Mfumo wa Uwekezaji na Ukuaji wa Tanzania, ESRF na UNDP zimefanikiwa kuibua miradi 69 ya kipaumbele yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni saba ndani ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa mpango huo.
Alisema miradi hiyo inahusisha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya utalii katika hifadhi za taifa, miradi ya maji, mamlaka za serikali za mitaa pamoja na miradi ya uchumi wa buluu.
“Tunataka mkutano huu uwe zaidi ya jukwaa la mazungumzo. Tumewaandalia wawekezaji na waandaaji wa miradi vikao maalumu vya ana kwa ana ili kufikia makubaliano yatakayowezesha upatikanaji wa mitaji na utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, Kapteni Hamadi Bakari Hamadi, alisema moja ya changamoto zinazoikabili Tanzania ni miradi mingi kushindwa kufikia kiwango cha kuvutia ufadhili kutoka kwa taasisi za fedha na wawekezaji wakubwa.
Alisema miradi mingi bado haijafikia hatua ya bankability, yaani kiwango kinachowezesha kukubalika na kufadhiliwa na taasisi za kifedha kutokana na maandalizi na uchambuzi wake kutokukidhi matakwa ya wawekezaji.
“Tunayo miradi mingi yenye fursa kubwa za uwekezaji, lakini changamoto ni mingi bado haijafikia hatua ya kuvutia taasisi za fedha na wawekezaji wakubwa. Tunahitaji kuiboresha ili iweze kufadhiliwa kwa urahisi,” alisema Kapteni Hamadi.
Alitaja mradi wa Bandari ya Mangapwani Zanzibar kuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayotafutiwa wawekezaji, akisema unatarajiwa kuwa na zaidi ya bandari nne na kuwa kichocheo kikubwa cha shughuli za uchumi wa bahari visiwani.
Kapteni Hamadi alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, taasisi za maendeleo na wataalamu wa uwekezaji ni muhimu katika kuhakikisha miradi hiyo inafikia kiwango cha kuvutia mitaji ya ndani na nje ya nchi.
Kwa ujumla, washiriki wa kongamano hilo walikubaliana kuwa TIGF ni moja ya mifumo muhimu itakayosaidia kuunganisha miradi ya maendeleo na vyanzo vya fedha, kuongeza ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuiwezesha Tanzania kufikia malengo makubwa yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.



Post a Comment