TANZANIA YAALIKWA KUWA MWENYEJI WA MAONESHO YA UFUGAJI NYUKI AFRIKA 2028

TANZANIA YAALIKWA KUWA MWENYEJI WA MAONESHO YA UFUGAJI NYUKI AFRIKA 2028

Na Arushadigital |ARGERIA

TANZANIA imepata heshima ya kualikwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya Tano ya Ufugaji wa Nyuki Afrika (Africa Bee Expo) yatakayofanyika mwaka 2028, yakitarajiwa kukutanisha wafugaji wa nyuki, wataalamu, watafiti na wawekezaji kutoka takribani nchi 50 duniani.


Mwaliko huo umetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Africa Bee Expo, Bw. Fatah Ben Chouia wa Algeria, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers.


Katika mazungumzo hayo, Bw. Chouia pia aliwasilisha mwaliko rasmi kwa Tanzania kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Nne ya Ufugaji wa Nyuki Afrika yatakayofanyika Algiers kuanzia Septemba 3 hadi 6, 2026, na kuhimiza taasisi za serikali, sekta binafsi pamoja na wadau wa ufugaji nyuki nchini kushiriki kikamilifu.


Akizungumza baada ya kupokea mialiko hiyo, Balozi Matinyi aliishukuru Africa Bee Expo kwa kuipa Tanzania heshima ya kuwa mgeni rasmi mwaka 2026 na mwenyeji wa maonesho ya mwaka 2028, akisema Serikali itaifanyia kazi fursa hiyo kwa lengo la kuendelea kuimarisha sekta ya ufugaji nyuki nchini.


Alisema sekta hiyo ni miongoni mwa maeneo yenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kutokana na kutoa ajira kwa zaidi ya Watanzania milioni mbili pamoja na kuchangia mapato ya nchi kupitia uzalishaji na biashara ya mazao ya nyuki.


Kwa upande wake, Bw. Chouia aliipongeza Tanzania kwa mafanikio yake makubwa katika ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa mazao yake, akibainisha kuwa nchi hiyo imejijengea sifa kubwa barani Afrika na duniani, hali iliyochangia kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo mwaka 2028.


Alisema maonesho hayo ni jukwaa muhimu linalowakutanisha wadau wa sekta ya ufugaji nyuki kutoka Afrika na maeneo mengine duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kuonesha teknolojia mpya, kujadili masuala ya uhifadhi wa nyuki na kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na sekta hiyo.


Maonesho hayo huambatana na kongamano la kimataifa la kitaalamu linalowaleta pamoja watafiti, wajasiriamali na wataalamu wa ufugaji nyuki kujadili maendeleo ya sekta hiyo na fursa mpya za uwekezaji.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Wafugaji Nyuki (Apimondia), Tanzania ni nchi ya pili kwa uzalishaji wa asali barani Afrika na ya kumi duniani, ikiwa na uzalishaji wa takribani tani 31,000 za asali na tani 1,800 za nta kila mwaka.

Hatua ya Tanzania kualikwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo mwaka 2028 inatajwa kuwa fursa muhimu ya kuitangaza nchi kimataifa, kuvutia uwekezaji katika sekta ya ufugaji nyuki na kufungua masoko mapya ya bidhaa za nyuki ndani na nje ya Afrika.

— Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania, Algiers, Algeria, Juni 3, 2026.

**ends**

Post a Comment

Previous Post Next Post