TAMONGSCO Yalia na Tozo Zilizofutwa, Yaituhumu Arusha Jiji na Arusha DC kwa Kutishia Kufunga Shule
Na Joseph Ngilisho| ARUSHA
SHIRIKISHO la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali Tanzania (TAMONGSCO) limeeleza wasiwasi wake kuhusu baadhi ya halmashauri nchini kuendelea kudai na kukusanya tozo ambazo tayari zimefutwa au kusamehewa kisheria kwa taasisi za elimu zisizo za serikali, huku likidai kuwa hali hiyo imejitokeza kwa kiwango kikubwa zaidi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Arusha DC).
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu uliofanyika jijini Arusha, Afisa Mtendaji Mkuu wa TAMONGSCO, Benjamin Nkonya, alisema baadhi ya shule na vyuo visivyo vya serikali vimekuwa vikikabiliwa na madai ya malipo ya tozo ambazo hazipaswi kutozwa kwa mujibu wa sheria, huku wengine wakitishiwa kufungiwa endapo hawatatekeleza madai hayo.
Alisema hali hiyo imeendelea kuwasababishia usumbufu mkubwa wamiliki na wasimamizi wa taasisi za elimu, ikiwalazimu kutumia muda na rasilimali nyingi kushughulikia migogoro ya kiutawala badala ya kujikita katika kuboresha utoaji wa elimu.
“Tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wanachama wetu katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu kuendelea kudaiwa tozo zilizofutwa au kusamehewa. Kinachotupa wasiwasi zaidi ni kwamba katika baadhi ya maeneo, hususan Arusha Jiji na Arusha DC, taasisi zimekuwa zikipewa vitisho vya kufungiwa iwapo hazitalipa tozo hizo,” alisema Nkonya.
Aliongeza kuwa mwenendo huo unaongeza gharama za uendeshaji wa taasisi za elimu na kuathiri juhudi za sekta binafsi katika kuunga mkono Serikali kupanua upatikanaji wa elimu bora nchini.
Nkonya alisisitiza kuwa TAMONGSCO inaamini katika uzingatiaji wa sheria na ulipaji wa kodi stahiki, akibainisha kuwa taasisi nyingi za elimu zisizo za serikali zimeendelea kutekeleza wajibu wao wa kikodi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Aidha, aliipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ushirikiano wake na wadau wa elimu pamoja na juhudi za kutoa elimu ya kodi, akisema uhusiano kati ya taasisi hizo na mamlaka hiyo umeendelea kuwa mzuri.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMONGSCO Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao, alisema uwekezaji katika sekta ya elimu unahitaji mazingira rafiki yatakayowezesha taasisi kufanya kazi kwa utulivu na ufanisi.
Alisema ni muhimu kwa mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha zinafuata sheria na miongozo iliyopo ili kuondoa migongano isiyo ya lazima ambayo inaweza kuathiri maendeleo ya sekta ya elimu na uwekezaji kwa ujumla.
“Tunachohitaji ni ushirikiano, uwazi na utekelezaji wa sheria kwa usawa. Taasisi za elimu zisizo za serikali ni wadau muhimu katika maendeleo ya elimu nchini, hivyo zinapaswa kupewa mazingira yanayowawezesha kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi,” alisema Mao.
Naye Wakili Mshauri wa TAMONGSCO, Paschal Temba, alisema sheria mbalimbali za fedha zimeweka bayana misamaha ya baadhi ya kodi na tozo kwa taasisi za elimu zisizo za serikali, ikiwemo leseni za biashara (Business Licence), Service Levy, tozo za mazingira na ada mbalimbali zinazotozwa na mamlaka za serikali za mitaa.
Alisema utekelezaji usiozingatia matakwa ya sheria unaweza kuleta mkanganyiko na migogoro kati ya wawekezaji katika sekta ya elimu na mamlaka za ukusanyaji wa mapato.
“Misamaha hii imewekwa kwa lengo la kuunga mkono utoaji wa huduma za elimu na kupunguza mzigo wa gharama kwa taasisi hizi. Ni muhimu mamlaka zote husika zikazingatia kikamilifu matakwa ya sheria ili kuondoa migongano inayoweza kuzorotesha uwekezaji katika elimu,” alisema Temba.
Kutokana na hali hiyo, TAMONGSCO imeiomba Serikali kufanya tathmini na ufuatiliaji wa kina kuhusu utekelezaji wa misamaha ya kodi na tozo katika halmashauri zote nchini, huku ikiitaka kuchukua hatua za haraka dhidi ya vitendo vya kuendelea kudai tozo zilizofutwa au kusamehewa kisheria.
Wadau hao wamesema hatua hiyo itasaidia kulinda mazingira ya uwekezaji katika sekta ya elimu, kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wanafunzi na kuhakikisha taasisi zisizo za serikali zinaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za taifa za kukuza elimu na maendeleo ya rasilimali watu.
***Ends***





Post a Comment