SAMIA AITAZAMA URUSI KAMA NGUZO YA USHIRIKIANO NA MAENDELEO YA TANZANIA
Na Joseph Ngilisho |Arushadigital| Moscow- URUSI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema ziara yake ya kiserikali nchini Urusi ina umuhimu mkubwa wa kihistoria kwa kuwa inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Urusi.
Rais Samia aliyasema hayo wakati wa mazungumzo rasmi na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ambapo alieleza kuwa ni zaidi ya nusu karne imepita tangu ziara ya mwisho ya kiongozi wa Tanzania nchini humo iliyofanywa mwaka 1969 na Baba wa Taifa, Julius Nyerere.
Alisema ziara hiyo ni fursa muhimu ya kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo endelevu kwa manufaa ya wananchi wa nchi zote mbili.
“Nina heshima kubwa kushukuru kwa mwaliko huu na mapokezi mazuri tuliyopatiwa. Ziara hii ni ya kihistoria kwangu binafsi na kwa taifa letu, kwani inakuja baada ya miaka mingi tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi,” alisema Rais Samia.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuishukuru Urusi kwa mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Afrika wakati wa miaka ya 1960, akieleza kuwa Tanzania imeendelea kunufaika na ushirikiano huo hadi sasa katika sekta mbalimbali za maendeleo.
“Urusi imekuwa mshirika muhimu wa Tanzania kwa muda mrefu. Mchango wake katika harakati za ukombozi wa Afrika na katika maendeleo ya nchi yetu unaonekana wazi, hivyo tunathamini sana urafiki huu wa kihistoria,” alisisitiza.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alimpongeza Rais Putin na wananchi wa Urusi kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Siku ya Ushindi (Victory Day), akieleza kuwa tukio hilo ni kumbukumbu muhimu ya uzalendo, mshikamano na kujitolea kwa wananchi wa Urusi.
Vilevile, alieleza kufurahishwa na fursa ya kutembelea makaburi ya mashujaa wa vita na kuweka shada la maua kwa heshima ya waliopigania uhuru na amani ya taifa hilo.
Rais Samia alisema Tanzania inaendelea kuamini kuwa ushirikiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia kwa manufaa ya wananchi wa mataifa hayo.
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi inatarajiwa kuimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi, huku viongozi hao wakijadili maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara, uwekezaji, elimu, nishati na maendeleo ya teknolojia.






Post a Comment