MUME ARUSHA ADAI KUNYANG’ANYWA MTOTO, KUPOTEZA MILIONI 12 NA KUBAMBIKIWA KESI YA KULAWITI MTOTO WAKE BAADA YA KIFO CHA MKEWE AFISA JWTZ, ADAI KUTESWA NA POLISI ARUSHA.
Na Joseph Ngilisho, ARUSHA
MKAZI wa Ngusero jijini Arusha, Richard Bonface, ameibuka na madai mazito akieleza kuwa maisha yake yamegeuka mateso tangu kufariki kwa mke wake, Martha Ngayega, aliyekuwa Afisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Kambi ya TMA Monduli.
Bonface alisema mke wake alifariki Machi 29, 2026 katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, lakini kabla hata ya kuzikwa tayari kulikuwa na migogoro iliyohusisha ndugu wa marehemu kuhusu masuala ya mazishi, mirathi na malezi ya mtoto wao wa pekee.
Akizungumza June 24,2016 Bonface alidai kuwa baada ya kurejea Arusha kutoka kwenye shughuli za mazishi, alikuta nyumba yake imevunjwa na kupekuliwa na watu aliowatambua kuwa maofisa wa JWTZ waliokuwa wakifuatilia sare za jeshi na vifaa vingine vilivyokuwa vinatumiwa na marehemu mke wake.
Alidai upekuzi huo ulifanyika siku moja baada ya mke wake kufariki dunia wakati mwili ukiwa bado haujazikwa.
“Nilipofika nyumbani nilikuta mlango wa chumba umevunjwa, nyumba imepekuliwa na vitu vikiwa vimetawanyika. Niliambiwa walikuwa wanatafuta sare za jeshi za marehemu,” alisema Bonface.
Bonface alidai kuwa upekuzi huo haukufuata taratibu za kisheria kwa kuwa haukuhusisha viongozi wa eneo husika wala mashuhuda wa Serikali za Mitaa.
“Hakukuwa na mwenyekiti wa mtaa, balozi wala mtendaji wa mtaa aliyeshuhudia tukio hilo. Ndiyo maana niliona kuna maswali mengi yanayohitaji majibu,” alidai.
Alisema wakati wa tukio hilo ndani ya nyumba kulikuwa na kiasi cha shilingi milioni 12 ambazo anadai zilikuwa mali ya marehemu mke wake, fedha ambazo hadi leo hajui zilipo.
Kutokana na hali hiyo, Bonface alisema aliamua kufikisha malalamiko yake kwa uongozi wa juu wa JWTZ jijini Dodoma akiomba uchunguzi ufanyike kuhusu mazingira ya upekuzi huo na upotevu wa fedha hizo.
Kwa mujibu wa Bonface, malalamiko yake yalipokelewa na baadaye maofisa waandamizi wa JWTZ walitumwa kufika nyumbani kwake Arusha kufanya tathmini ya tukio hilo.
“Walifika nyumbani kwangu, wakashuhudia mlango uliovunjwa, wakakagua nyumba na kuona namna ilivyokuwa imepekuliwa. Walichukua maelezo yangu na kufanya uchunguzi wao,” alisema.
Bonface alidai kuwa baadaye maofisa wa JWTZ waliohusishwa na upekuzi huo waliitwa Dodoma na kuhojiwa na viongozi wao kuhusu mazingira ya operesheni hiyo pamoja na madai ya kutoweka kwa fedha hizo.
Hata hivyo, alisema hadi sasa hajawahi kupewa mrejesho wa kina kuhusu matokeo ya uchunguzi huo wala kurejeshewa fedha anazodai zilipotea.
“Nina zaidi ya mwaka mmoja sasa nikisubiri haki yangu. Fedha hizo sijaziona mpaka leo na sijapata maelezo ya kuridhisha kuhusu kilichotokea,” alisema.
Mbali na madai ya upotevu wa fedha, Bonface alisema nyaraka mbalimbali muhimu ikiwemo cheti cha ndoa, nyaraka za mtoto wao na hati nyingine za familia zilichukuliwa katika mazingira ambayo bado yanamtilia shaka.
Bonface pia alidai kuwa baada ya mazishi aliingia kwenye mgogoro mkubwa na baadhi ya ndugu wa marehemu ambao anadai waliratibu njama za kumchafua kwa kumbambikizia tuhuma za kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kumzaa.
Kwa mujibu wa Bonface, taarifa hizo zilisambazwa kupitia vyombo vya habari baada ya mwandishi mmoja kudaiwa kurubuniwa na watu waliokuwa na tofauti naye.
Alisema baada ya taarifa hizo kusambazwa, alikamatwa jijini Dodoma na kusafirishwa hadi Arusha akiwa amefungwa pingu mikononi kwa ajili ya uchunguzi.
“Nilikamatwa Dodoma na kuletwa Arusha kama mhalifu mkubwa. Nilipofikishwa kituoni nilihojiwa na kuteswa kwa madai kwamba nimemlawiti mtoto wangu,” alidai Bonface.
Katika madai yake, Bonface alimtaja Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya ya Arusha, Omari Mahita, kuwa miongoni mwa maofisa waliomhoji kwa ukali wakati wa uchunguzi huo.
Hata hivyo, alisema mama yake mzazi alilazimika kumrejesha mtoto huyo Arusha kutoka Mwanza alikokuwa amepelekwa baada ya mazishi ya marehemu ili afanyiwe uchunguzi wa kitabibu.
Bonface alisema mtoto alipimwa katika hospitali mbili tofauti jijini Arusha na matokeo yalionyesha kuwa hakukuwa na dalili zozote za kuingiliwa kingono.
Alidai kuwa baada ya majibu hayo, polisi walimwachia huru kutokana na kutokuwepo ushahidi wa kuthibitisha tuhuma zilizokuwa zikimkabili.
Pamoja na kuachiwa huru, Bonface anasema hakuruhusiwa kurejea kuishi na mtoto wake ambaye kwa sasa analelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima.
“Ninaumia sana kuona mwanangu analelewa kituo cha watoto yatima wakati mimi baba yake mzazi nipo hai. Naiomba Serikali iingilie kati ili nirejeshewe mtoto wangu,” alisema.
Bonface anadai kuwa baadhi ya ndugu wa marehemu wanatumia mbinu mbalimbali za kumtenga na mtoto huyo kwa lengo la kumnyima haki zake kama mzazi na mume halali wa marehemu.
Alisema yeye na Martha Ngayega walifunga ndoa takatifu Desemba 12, 2016 na walibahatika kupata mtoto mmoja pekee.
Aidha, anahisi kuwa migogoro hiyo inahusishwa na masuala ya mafao na mirathi yanayotokana na utumishi wa marehemu ndani ya JWTZ, akidai kuwa kuna watu wanaotaka kumzuia yeye na mtoto wake kunufaika na haki zinazostahili kwa mujibu wa sheria.
Bonface ameomba Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka za ustawi wa jamii kuingilia kati ili uchunguzi wa madai yake ukamilike na haki itendeke.
“Ninaomba Serikali inisaidie. Nataka ukweli ujulikane kuhusu fedha zilizopotea, mtoto wangu arejee mikononi mwangu kama sheria inavyoruhusu na haki yangu kama mume wa marehemu iheshimiwe,” alisema.
Hata hivyo, madai haya ni upande mmoja wa simulizi la Richard Bonface. Jitihada za hili kupata maelezo kutoka kwa ndugu wa marehemu, JWTZ, Jeshi la Polisi pamoja na mamlaka za ustawi wa jamii kuhusu tuhuma hizo zinaendelea ili kupata upande wao wa tukio hili.




Post a Comment