MONDI AIPONGEZA SERIKALI KWA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI,AIOMBA SERIKALI KUENDELEA KUWAUNGANISHA NA WAWEKEZAJI WA NJE

WAWEKEZAJI WA NDANI WANUFAIKA NA JUKWAA LA UWEKEZAJI, WAIOMBA SERIKALI KUENDELEA KUWAUNGANISHA NA WAWEKEZAJI WA NJE

Na Joseph Ngilisho | Arusha

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mondi LTD na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Dar es Salaam na Pwani (DACOREMA), Francis Mondi, amesema majukwaa ya uwekezaji yanayoandaliwa na serikali yana mchango mkubwa katika kukuza biashara za wawekezaji wa ndani kwa kuwapatia fursa za kujifunza, kushirikiana na kupata mitaji kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wa uwekezaji  jijini Arusha, Mondi alisema wawekezaji wa ndani wanaendelea kunufaika na uwepo wa wawekezaji wa kimataifa, taasisi za kifedha na wadau wengine wanaoshiriki katika majukwaa hayo kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji na maendeleo ya uchumi.

Alisema serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kufungua milango ya uwekezaji kwa kuwakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, jambo ambalo limeongeza matumaini kwa sekta binafsi.

"Tunashukuru sana serikali yetu kwa kutuletea fursa kama hizi. Tumekutana na wawekezaji mbalimbali, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo wanaotangaza fursa za uwekezaji. Hii inatupa nafasi ya kujifunza na kuangalia maeneo mapya ya kukuza biashara zetu," alisema Mondi.

Alieleza kuwa moja ya mafanikio makubwa yanayotokana na majukwaa hayo ni kupanua wigo wa biashara kwa kupata taarifa za miradi na maeneo mapya ya uwekezaji yanayopatikana sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo Zanzibar na maeneo mengine yenye fursa za kiuchumi.

"Tunapanua wigo wa biashara zetu. Tumesikia kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta tofauti, hivyo tutafuatilia kwa kina taarifa hizo ili kuona maeneo yanayolingana na shughuli zetu za ujenzi, usafirishaji na uchimbaji wa madini," alisema.

Mondi aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje unasaidia kuongeza maarifa, teknolojia na mbinu bora za uendeshaji wa biashara, jambo linalochochea ukuaji wa sekta binafsi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

"Tunapokutana na wawekezaji wa nje tunapata uzoefu na ujuzi mkubwa zaidi. Maarifa hayo yanatusaidia kuboresha biashara zetu na kutufanya tuwe na ushindani mkubwa zaidi katika soko," alisema.

Aidha, aliishauri serikali kuendelea kuandaa makongamano na majukwaa ya uwekezaji mara kwa mara ili kutoa nafasi kwa wawekezaji wa ndani kujifunza zaidi na kujenga ushirikiano wa kimataifa unaoweza kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.

"Tunaomba serikali iendelee kutupatia elimu na fursa kama hizi. Majukwaa haya yana manufaa makubwa kwa wawekezaji wa ndani na yanasaidia kufungua milango mipya ya biashara na uwekezaji. Tunaamini yataendelea kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi yetu," alisema Mondi.

Ends..

Post a Comment

Previous Post Next Post

Contact Form