LUKUMAY AIHOJI SERIKALI KUHUSU FIDIA YA SHULE YA SEKONDARI ILKIDING’A
Na Joseph Ngilisho-Arushadigital| DODOMA
Akichangia leo June 2,2026 katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Dkt. Lukumay alisema Serikali ilifanya tathmini ya mali za wananchi waliopisha eneo la shule hiyo, ambapo thamani ya fidia iliyobainishwa ilikuwa zaidi ya Shilingi milioni 295 hadi milioni 300, lakini hadi sasa hakuna malipo yaliyofanyika.
Alisema hali hiyo imewalazimu baadhi ya wananchi kuendelea kuishi ndani ya eneo la shule wakisubiri kulipwa stahiki zao kabla ya kuondoka na kuachia eneo lote kwa matumizi ya elimu.
Mbunge huyo alihoji ni lini Serikali itakuwa tayari kuwalipa fidia wananchi hao ili waweze kuondoka katika eneo hilo na kutoa nafasi kwa shule kufanya kazi zake bila changamoto za umiliki wa ardhi.
Akijibu swali hilo, Serikali ilikiri umuhimu wa kulipa fidia kwa wananchi wanaotoa maeneo yao kwa ajili ya huduma za jamii na kueleza kuwa suala hilo litafuatiliwa kwa karibu ili kuhakikisha haki inatendeka.
“Mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha tunaendelea kuboresha miundombinu na huduma za kijamii nchini. Hata hivyo, kwa maeneo ambayo Serikali imechukua kwa ajili ya huduma za jamii kama elimu, upo utaratibu wa kisheria wa kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili,” ilieleza Serikali.
Serikali ilisema italichukua suala hilo na kulifuatilia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na Halmashauri ya Arusha ili kubaini hatua zinazoweza kuchukuliwa kuhusu malipo ya fidia hiyo.
“Tutafuatilia suala hili kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Halmashauri ya Arusha ili kuona kama halmashauri inaweza kupata uwezo wa kulipa fidia hiyo. Endapo itabainika kuwa halmashauri haiwezi kumudu gharama hizo, Serikali itaangalia utaratibu mwingine wa kuhakikisha wananchi hao wanalipwa fidia na kupata haki zao,” ilisisitiza.
Aidha, Serikali ilitambua mchango wa wananchi wa Ilkiding’a ambao walitoa maeneo yao kwa dhamira njema ya kuendeleza sekta ya elimu katika eneo hilo, na kusisitiza kuwa juhudi zao zinapaswa kuthaminiwa kwa kuhakikisha wanapatiwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.
Kauli hiyo imeibua matumaini mapya kwa wananchi wa Ilkiding’a ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri malipo ya fidia, huku wakitaka suala hilo kupatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuondoa mgogoro wa matumizi ya eneo la shule na kuwezesha mazingira bora ya utoaji wa elimu.
Ends


