MAGENDO KUPITIA BANDARI BUBU TANGA YAPUNGUA KWA KIASI KIKUBWA – RC BURIAN
Na Hadija Bagasha, Tanga
Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya vyombo vya ulinzi na usalama, TRA, taasisi nyingine za Serikali pamoja na wadau wa sekta ya biashara, ambao wameendelea kushirikiana kubaini na kudhibiti njia zinazotumiwa kuingiza bidhaa za magendo nchini.
"Mapambano dhidi ya magendo si jukumu la Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa kila mdau. Tunapoimarisha udhibiti wa bidhaa zinazoingizwa kinyume cha sheria, tunalinda uchumi wa Taifa na kuongeza mapato yanayowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo," alisema.
Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kuwa wazalendo kwa kulipa kodi stahiki na kuachana na vitendo vya ukwepaji kodi, akisisitiza kuwa kodi ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kupitia ujenzi wa barabara, shule, vituo vya afya, hospitali na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga, CPA Castro John, alisema katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996, TRA imepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, hali iliyoimarisha uwezo wa Serikali kugharamia miradi na huduma mbalimbali za maendeleo.
Alisema makusanyo ya kodi nchini yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 531 katika mwaka wa fedha 1996/1997 hadi kufikia Shilingi trilioni 32 katika mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayoakisi mafanikio ya mageuzi yaliyofanyika katika mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa kodi.
CPA Castro alibainisha kuwa mafanikio hayo yamechochewa na matumizi ya teknolojia za kisasa, uboreshaji wa mifumo ya kidijitali, utoaji wa elimu kwa walipa kodi na kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya TRA na wafanyabiashara.
Alisisitiza kuwa TRA itaendelea kuwekeza katika teknolojia, kupanua wigo wa walipa kodi, kuboresha huduma kwa walipa kodi na kujenga mazingira rafiki ya ulipaji kodi ili kuongeza mapato ya Serikali na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yamekuwa jukwaa la kutathmini mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996, huku yakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wananchi katika kujenga mfumo imara wa ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya Taifa.





Post a Comment