KARIBU KILIFAIR 2026 YAZIDI KUNG'ARA, YAFUNGUA FURSA ZA UTALII, UWEKEZAJI NA BIASHARA TANZANIA
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu Kilifair 2026 yameendelea kuthibitisha nafasi yake kama jukwaa kubwa la utalii na uwekezaji Afrika Mashariki, huku yakichangia kuitangaza Tanzania kimataifa, kuvutia wawekezaji, kuongeza biashara za utalii na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi.
Akifungua rasmi maonesho hayo katika Viwanja vya Magereza jijini Arusha kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Utalii nchini, Dkt. Thereza Mugobi, alisema Karibu Kilifair imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuitangaza Tanzania duniani na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara katika sekta ya utalii.
Alisema ushiriki wa zaidi ya waoneshaji 1,560 na wanunuzi wa huduma za utalii zaidi ya 500 kutoka nchi zaidi ya 40 unaonesha imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa inaendelea kuwa nayo kwa Tanzania kama moja ya destinasheni bora za utalii na uwekezaji duniani.
“Sekta ya utalii inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa kwa kuchangia takribani asilimia 17.2 ya Pato la Taifa na kutoa ajira zaidi ya milioni 2.5 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania,” alisema Dkt. Mugobi.
Alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya utalii imepata mafanikio makubwa kutokana na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu, uboreshaji wa huduma, utangazaji wa vivutio vya utalii na upanuzi wa masoko mapya ya utalii duniani.
Kwa mujibu wake, mapato ya sekta hiyo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi zaidi ya dola bilioni 4.4 kwa sasa, hali inayodhihirisha ukuaji mkubwa wa sekta hiyo katika kipindi cha miaka michache iliyopita.
Dkt. Mugobi alisema Tanzania inaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kisasa kuitangaza nchi, ikiwemo filamu ya “Tanzania: The African Dream”, ambayo imekuwa sehemu ya mkakati wa kuonesha uzuri wa vivutio vya Tanzania kwa hadhira ya kimataifa.
“Filamu hii inaonesha mchanganyiko wa kipekee wa vivutio vya Tanzania kuanzia wanyamapori, tamaduni, mandhari ya asili, fukwe, watu na urithi wa kihistoria. Tunaamini itawahamasisha mamilioni ya watu duniani kuichagua Tanzania kama destinasheni yao ya safari,” alisema.
Aliongeza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee duniani ikiwemo Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro, fukwe za Zanzibar pamoja na vivutio vya ukanda wa kusini na maeneo ya urithi wa utamaduni yanayovutia wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Karibu Kilifair, Dominick Shoo, alisema maonesho hayo yanaendelea kukua kwa kasi na kuimarisha nafasi yake kama jukwaa kubwa la biashara za utalii katika Afrika Mashariki.
Alisema mwaka huu maonesho hayo yamehusisha waoneshaji 550 kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani, ikilinganishwa na waoneshaji 500 wa mwaka uliopita.
Aidha, alisema zaidi ya wanunuzi 1,000 wa huduma za utalii kutoka nchi zaidi ya 30 wamejitokeza kushiriki maonesho hayo, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa ushawishi wa Karibu Kilifair katika soko la kimataifa.
“Karibu Kilifair si maonesho ya kawaida tu, bali ni jukwaa la kimkakati linalochangia juhudi za Serikali za kukuza utalii. Tunawapa mawakala wa safari, waendeshaji wa utalii na wanunuzi wa kimataifa nafasi ya kuifahamu Tanzania moja kwa moja na kuwa mabalozi wa kuitangaza duniani,” alisema Shoo.
Alisema kutokana na ongezeko la washiriki na mahitaji ya biashara, waandaaji wameanzisha siku maalum ya nne kwa ajili ya mikutano ya kibiashara (B2B Networking Day), inayowapa washiriki muda zaidi wa kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutafuta fursa mpya za biashara.
Shoo pia alieleza kuwa maonesho hayo yameanzisha programu ya Country Days inayolenga kutangaza utamaduni wa nchi za Afrika Mashariki kupitia muziki, ngoma za asili, vyakula, sanaa na urithi wa kitamaduni, huku siku ya ufunguzi ikiadhimishwa kama Tanzania Day.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendeshaji wa Utalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo, alisema Karibu Kilifair imeendelea kuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha wadau wa utalii, wafanyabiashara na wanunuzi wa kimataifa kwa manufaa ya sekta hiyo.
Alisema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara za utalii kwa kuwapa wafanyabiashara wa ngazi zote fursa ya kukutana moja kwa moja na wanunuzi kutoka mataifa mbalimbali.
“Karibu Kilifair imekuwa sehemu muhimu ya kutangaza Tanzania na kuleta wanunuzi wa kimataifa. Hii inasaidia kukuza biashara na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi yetu,” alisema Chambulo.
Aliongeza kuwa ushiriki mkubwa wa wanunuzi wa kimataifa unaonesha imani waliyonayo kwa Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani, huku akitabiri kuwa maonesho ya mwaka 2027 yatakuwa makubwa zaidi kutokana na ongezeko la washiriki na fursa za biashara.
Wakati huo huo, Kampuni ya kimataifa ya huduma za malipo ya kidijitali ya Visa imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya malipo ya kisasa ili kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii.
Akizungumza katika maonesho hayo, mwakilishi wa Visa, Vikta Makene, alisema Tanzania imeendelea kurekodi mafanikio makubwa katika utalii, huku Zanzibar ikitajwa miongoni mwa maeneo yaliyopata ukuaji mkubwa zaidi wa watalii duniani baada ya janga la UVIKO-19.
Makene alisema idadi ya watalii wa kimataifa waliotembelea Zanzibar imeongezeka kutoka takribani milioni moja mwaka 2021 hadi zaidi ya milioni mbili mwaka 2024, huku mapato ya utalii yakiongezeka kwa kasi na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika uchumi wa taifa.
Alisema Visa imeendelea kusaidia maendeleo ya sekta hiyo kwa kuwezesha malipo salama, rahisi na yanayokubalika kimataifa kwa watalii na wafanyabiashara.
“Tunao uhakika kuwa miaka bora zaidi ya utalii Tanzania bado ipo mbele yetu, na Visa imejipanga kuwa sehemu ya mafanikio hayo kwa kuhakikisha malipo ya kidijitali yanakuwa rahisi, salama na yanayopatikana kwa wote,” alisema.
Dkt. Mugobi alihitimisha kwa kusema kuwa Karibu Kilifair si maonesho ya kawaida bali ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa utalii wa Tanzania, kwani mahusiano ya kibiashara yanayojengwa kupitia maonesho hayo yanachangia kuongeza watalii, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, alisema Tanzania inaendelea kujiandaa kutumia kikamilifu fursa ya kuandaa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kwa ushirikiano na Kenya na Uganda, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika miundombinu, teknolojia za kidijitali, ubora wa huduma na kampeni za masoko ili kuhakikisha sekta ya utalii inanufaika kikamilifu na tukio hilo la kihistoria.
Maonesho ya Karibu Kilifair yameendelea kujidhihirisha kama moja ya matukio makubwa zaidi ya utalii katika Afrika Mashariki, yakikusanya pamoja waoneshaji, wanunuzi wa huduma za utalii, wawekezaji na wadau mbalimbali kutoka duniani kote kwa lengo la kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano katika sekta ya utalii.
Ends..


Post a Comment