LUKUMAY AMPONGEZA RAIS SAMIA KWA HESHIMA YA KIMATAIFA, ASEMA AMEIINUA TANZANIA DUNIANI
Na Joseph Ngilisho | ARUSHA
MBUNGE wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiletea Tanzania heshima kubwa katika jukwaa la kimataifa kupitia tuzo na shahada za heshima anazoendelea kutunukiwa kutokana na mchango wake katika maendeleo ya jamii, elimu, afya na diplomasia.
Dkt. Lukumay alitoa pongezi hizo leo Juni 5, 2026, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ngaramtoni, wilayani Arumeru mkoani Arusha, uliohudhuriwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, akiwa katika ziara ya kikazi ya kuzungumza na wananchi na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Alisema kutambuliwa kwa Rais Samia na taasisi mbalimbali za kimataifa ni uthibitisho wa uongozi wake mahiri ambao umeifanya Tanzania kuendelea kupata heshima na ushawishi mkubwa katika Jumuiya ya Afrika na dunia kwa ujumla.
Dkt. Lukumay alimpongeza Rais Samia kwa kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu cha Urafiki wa Watu wa Urusi (RUDN University) cha jijini Moscow, nchini Urusi, akisema heshima hiyo ni matokeo ya mchango wake mkubwa katika kuimarisha elimu, maendeleo ya kijamii, diplomasia na ushirikiano wa kimataifa.
Alisema kutunukiwa kwa Rais Samia shahada hiyo na moja ya vyuo vikuu vinavyoheshimika duniani kunaonesha namna ambavyo Tanzania imeendelea kujijengea hadhi kubwa katika jumuiya ya kimataifa kupitia uongozi wake.
"Kwa niaba ya wananchi wa Arumeru Magharibi tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima na Chuo Kikuu cha RUDN nchini Urusi pamoja na tuzo nyingine mbalimbali za kimataifa. Hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaonesha kuwa dunia inatambua kazi kubwa anayofanya katika kuwaletea maendeleo Watanzania," alisema Dkt. Lukumay.
Mbunge huyo aliongeza kuwa mbali na kutunukiwa shahada hiyo, Rais Samia pia ameendelea kutambuliwa katika ngazi za kimataifa kutokana na juhudi zake za kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na mchango wake katika maendeleo ya kijamii barani Afrika.
Alisema mafanikio hayo yanaenda sambamba na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini, ikiwemo uwekezaji katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu ambayo imeendelea kuboresha maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Arumeru Magharibi.
Dkt. Lukumay alibainisha kuwa uongozi wa Rais Samia umeleta matumaini mapya kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi inayogusa maisha yao moja kwa moja huku Tanzania ikiendelea kuimarisha mahusiano yake na mataifa mbalimbali duniani.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi zake za kuijenga Tanzania yenye uchumi imara, huduma bora za kijamii na maendeleo jumuishi kwa wote.
"Tunajivunia kuwa na Rais ambaye kazi zake zinatambuliwa ndani na nje ya nchi. Huu ni ushahidi kuwa Tanzania inaendelea kusonga mbele na kupata heshima kubwa duniani kutokana na uongozi wake wenye maono na matokeo chanya kwa wananchi," alisema Dkt. Lukumay.
Ends

Post a Comment