DAKTARI BINGWA WA KINYWA NA MENO KUTOKA UJERUMANI KUTUA TANZANIA KUTOA HUDUMA NA MAFUNZO YA BURE, WANANCHI ARUMERU MAGHARIBI KUNUFAIKA

DAKTARI BINGWA WA KINYWA NA MENO KUTOKA UJERUMANI KUTUA TANZANIA-ARUMERU MAGHARIBI KUTOA HUDUMA NA MAFUNZO YA BURE

Na Joseph Ngilisho | ARUSHADIGITAL 

Daktari Bingwa wa Afya ya Kinywa na Meno kutoka nchini Ujerumani, Dkt. Ursula Elizabeth, anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania Julay 20-25 kwa ziara maalumu ya kibinadamu inayolenga kutoa huduma za afya ya kinywa na meno pamoja na mafunzo kwa jamii kupitia programu ya Dento Outreach.


Katika ziara hiyo, Dkt. Ursula Elizabeth atatembelea maeneo mbalimbali mkoani Arusha ikiwemo Gereza la Arusha, vituo vya kulelea wazee, shule za wanafunzi, pamoja na makundi maalumu ya kijamii yakiwemo vituo vya watoto yatima, ambapo atatoa elimu ya afya ya kinywa na meno pamoja na huduma za matibabu bure kwa wananchi.


Programu hiyo inalenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kinga, usafi na matunzo sahihi ya afya ya kinywa na meno, sambamba na kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa huduma za kitaalamu ambao mara nyingi hukumbana na changamoto za upatikanaji wa huduma hizo.


Mbali na utoaji wa huduma za afya, Dkt. Ursula Elizabeth kwa kushirikiana na timu yake pamoja na Mbunge wa Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, wanatarajia kuanzisha fursa mbalimbali za mafunzo na maendeleo ya taaluma kwa vijana na wataalamu wa afya ya kinywa nchini.


Kupitia ushirikiano huo, baadhi ya wataalamu wa afya ya kinywa na meno kutoka Tanzania wanatarajiwa kupata nafasi za mafunzo ya kibobezi nchini Ujerumani, huku wengine wakinufaika na fursa za ajira katika sekta ya afya nchini humo.


Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi ya Dento Outreach, ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za afya ya kinywa nchini pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa Kitanzania kupitia kubadilishana uzoefu na wataalamu wa kimataifa.


Wadau wa sekta ya afya wameeleza kuwa ujio wa Dkt. Ursula Elizabeth ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno nchini, hususan katika Jimbo la Arumeru Magharibi ambako baadhi ya wananchi wamekuwa wakikabiliwa na athari za matumizi ya maji yenye kiwango kikubwa cha madini ya fluoride.


Aidha, ujio huo unatarajiwa kufungua milango ya ushirikiano wa kimataifa katika nyanja za mafunzo, ajira na utoaji wa huduma za afya, hatua ambayo itachangia kuinua kiwango cha huduma za afya ya kinywa na meno nchini Tanzania.

Ends .

Post a Comment

Previous Post Next Post