TPA: Tozo Mpya ya Miundombinu ya Bandari Kufungua Enzi Mpya ya Uchukuzi na Biashara
Na Hadija Bagasha, Arushadigital |Tanga
MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA) imesema kuanzishwa kwa Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari (Port Infrastructure Development Levy – PID) kutakuwa chachu ya maboresho makubwa katika sekta ya usafirishaji wa mizigo nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma bandarini, kupunguza gharama kwa wafanyabiashara na kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.Tozo hiyo mpya inatarajiwa kuanza rasmi kutumika Julai Mosi mwaka huu baada ya kuahirishwa kutoka Machi kufuatia maoni ya wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara waliotaka muda zaidi wa kutoa mapendekezo yao kuhusu utekelezaji wake.
Akizungumza jijini Tanga katika kikao cha ushirikishwaji wa wadau kuhusu utekelezaji wa tozo hiyo, Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega alisema ongezeko kubwa la shehena katika bandari mbalimbali nchini limeifanya Serikali kuona umuhimu wa kuwekeza zaidi katika upanuzi na uboreshaji wa miundombinu ya bandari ili kuendana na kasi ya ukuaji wa biashara.
Alisema kwa sasa Bandari ya Tanga inapokea na kuhudumia takribani tani milioni mbili za mizigo kwa mwaka, huku makadirio yakionesha kuwa miundombinu iliyopo inaweza kufikia ukomo wake kabla ya mwaka 2030 kutokana na ongezeko kubwa la matumizi ya bandari hiyo.
“Mahitaji ya huduma za bandari yanaongezeka kwa kasi kubwa, hivyo maboresho ya miundombinu ni jambo lisiloepukika kama tunataka kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi,” alisema Mbega.
Mbega alifafanua kuwa fedha zitakazokusanywa kupitia PID zitaelekezwa katika miradi ya kimkakati ya maendeleo ya bandari, ikiwemo ujenzi wa gati jipya katika Bandari ya Tanga pamoja na kuendelezwa kwa eneo la Mwambani kuwa bandari kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia meli kubwa zaidi za kimataifa.
Alisema kwa sasa Bandari ya Tanga ina magati mawili pekee, lakini kuna mpango wa kujenga gati la tatu lenye urefu wa mita 900 ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa kwa wakati mmoja.
“Eneo la Mwambani lina nafasi kubwa ya kuwa bandari ya kisasa yenye zaidi ya magati 10, jambo litakaloifanya Tanga kuwa lango muhimu la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbega, maboresho hayo yataongeza ushindani wa bandari za Tanzania katika soko la kikanda na kimataifa, sambamba na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta za usafirishaji, biashara na viwanda.
Aidha alisema ucheleweshaji wa huduma bandarini umekuwa ukiwasababishia wafanyabiashara hasara kubwa kutokana na baadhi ya meli kulazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kupakia au kupakua mizigo.
“Meli inapokaa nje ya bandari hulipiwa hadi dola za Marekani 20,000 kwa siku. Mwisho wa siku gharama hizi humgusa mfanyabiashara na hata mwananchi wa kawaida kupitia kupanda kwa gharama za bidhaa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mbega alisema maboresho yaliyofanywa katika reli ya Tanga yenye thamani ya Sh bilioni 429.1 yamefungua fursa mpya za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi za Rwanda na Burundi kupitia reli hiyo ambayo kwa muda mrefu ilikuwa haitumiki kikamilifu.
Hata hivyo alikiri kuwa ongezeko la matumizi ya reli hiyo limeibua changamoto mpya ya upungufu wa mabehewa kutokana na idadi kubwa ya wateja wanaohitaji huduma hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TACAS), Ephraim Mwankusye alisema wadau wengi wa sekta ya usafirishaji wanaunga mkono utekelezaji wa tozo hiyo kwa kuwa italeta mageuzi makubwa katika huduma za bandari nchini.
Alisema fedha zitakazopatikana kupitia PID zinatarajiwa kusaidia kuboresha Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na kuharakisha maendeleo ya Bandari ya Bagamoyo na miundombinu ya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini.
“Lengo ni kuwa na bandari za kisasa zenye uwezo wa kuhudumia mizigo mingi kwa haraka zaidi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda,” alisema Mwankusye.
Naye Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa TACAS, Vicent Mwamakigula alisema kuanzishwa kwa tozo hiyo kumekuja wakati muafaka kwa kuwa kutaharakisha maboresho ya miundombinu katika Bandari ya Tanga na kuimarisha huduma za usafirishaji wa mizigo.
Alisema maboresho hayo yataongeza ushindani wa Bandari ya Tanga, kuvutia wawekezaji zaidi na kusaidia kupunguza gharama za usafirishaji kwa wafanyabiashara huku wananchi wakinufaika kupitia ongezeko la ajira na shughuli za kiuchumi.
Kwa ujumla, utekelezaji wa Tozo ya Maendeleo ya Miundombinu ya Bandari unaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kupitia bandari zenye uwezo wa kisasa na huduma zenye ushindani mkubwa.


0 Comments