TARURA LONGIDO YAOMBA BILIONI 2.3 KUBORESHA BARABARA
Na Joseph Ngilisho|LONGIDO
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) Wilaya ya Longido umeomba kutengewa zaidi ya shilingi bilioni 2.3 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kuboresha na kufanya matengenezo ya barabara mbalimbali huku ukikabiliwa na changamoto ya ucheleweshaji wa fedha na uharibifu wa miundombinu unaosababishwa na mvua kubwa.
Taarifa hiyo iliwasilishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido na Kaimu Meneja wa TARURA wilayani humo, Rogers Kifunda, aliyesema taasisi hiyo kwa sasa inahudumia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 695.81 huku maombi ya kuongeza mtandao huo hadi kilomita 1025.9 yakiwa yamewasilishwa TARURA makao makuu.
Kifunda alisema licha ya jitihada zinazoendelea, utekelezaji wa miradi ya barabara bado unakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa fedha kwa wakati pamoja na mvua kubwa zinazosababisha uharibifu wa barabara katika maeneo kadhaa ya wilaya hiyo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2024/2025, TARURA inaendelea kutekeleza miradi miwili ya maendeleo ya barabara ambapo mmoja wa miradi hiyo unaotekelezwa katika kata za Longido na Orbomba umefikia asilimia 75 ya utekelezaji.
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Nemdende Construction kwa gharama ya shilingi milioni 286.
Aidha, alisema mradi mwingine unaofadhiliwa na Benki ya Dunia katika Kata ya Kimokouwa, Kitongoji cha Matianii, umekamilika kwa asilimia 100.
Kwa upande wa mwaka wa fedha 2025/2026, alisema TARURA imeanza utekelezaji wa miradi mingine miwili ambapo mmoja wake unatekelezwa na kampuni ya Rich Junior Engineering katika kata za Longido, Orbomba, Mundarara, Mairouwa na Matale.
Alisema hadi sasa mkandarasi huyo amefikia asilimia 50 ya utekelezaji wa mradi wa lami wenye thamani ya shilingi milioni 395 unaendelea.
Katika kikao hicho, baadhi ya madiwani waliipongeza TARURA kwa juhudi zinazofanywa kuboresha miundombinu ya barabara huku wakisisitiza umuhimu wa kuongeza fedha ili kuondoa changamoto za usafiri na usafirishaji zinazowakabili wananchi.
Hata hivyo, baadhi ya madiwani walionesha kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa matengenezo ya barabara katika maeneo yao na kutishia kumwadhimia kutokuwa na imani na Meneja wa TARURA wilayani humo kutokana na kusuasua kwa miradi hiyo.
Diwani wa Kata ya Elang’ata Dapashi, Alex Logotu,alilalamikia ubovu wa barabara katika kata yake akidai kuwa matengenezo hayajawahi kufanyika kwa muda mrefu hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido,Thomas Ngobei, aliitaka TARURA kuhakikisha barabara zote za kata zinaunganishwa katika mtandao rasmi wa barabara ili kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Ngobei ambaye pia ni diwani wa kata ya Longido, alisema kutokana na kutokuwepo kwa baadhi ya taarifa za taasisi katika kikao hicho, mjadala wa kina kuhusu utekelezaji wa miradi utaendelea katika vikao vijavyo ili kutoa nafasi kwa wajumbe kujadili changamoto na mafanikio ya taasisi mbalimbali.
ENDS..




0 Comments