MBUNGE LUKUMAY AIKABA KOO SERIKALI KUHUSU UKOSEFU WA GARI KWA MAAFISA KILIMO ARUMERU MAGHARIBI,ATAKA WAZIRI AMBARANE KUJIONEA

 MBUNGE WA ARUMERU MAGHARIBI AIOMBA SERIKALI KUPELEKA GARI KWA MAAFISA KILIMO

Na Joseph Ngilisho|DODOMA 

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay ameiiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kuhakikisha inapeleka gari kwa ajili ya maafisa kilimo katika jimbo hilo ili kuwawezesha kuwafikia wananchi kwa urahisi na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.

Akichangia bungeni, Dkt. Lukumay alisema wananchi wengi wa Arumeru Magharibi wanategemea shughuli za kilimo na ufugaji, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa wataalamu wanaoweza kuwafikia mashambani kutokana na uhaba wa vitendea kazi, hususan usafiri.

Alisema gari lililopo kwa sasa ni bovu hali inayosababisha maafisa kilimo kushindwa kuwafikia wananchi kwa wakati na kutoa huduma muhimu za kitaalamu zinazohitajika kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.

“Wananchi wengi ni wakulima na wanahitaji ushauri wa wataalamu wa kilimo mara kwa mara, lakini wataalamu hawa hawawezi kuwafikia kwa sababu hawana usafiri wa uhakika. Gari lililopo ni bovu,” alisema Dkt. Lukumay.

Aidha, mbunge huyo aliiomba Serikali kuzingatia mahitaji ya Arumeru Magharibi wakati wa ugawaji wa magari mapya yanayonunuliwa na Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kurahisisha shughuli za maafisa kilimo nchini.

Akijibu hoja hiyo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde alisema Serikali imeendelea kununua magari pamoja na pikipiki kwa ajili ya maafisa kilimo na maafisa ushirika ili kuboresha huduma za ugani katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema tayari Serikali imeshagawa magari katika baadhi ya mikoa na inaendelea kuongeza magari mengine mapya yatakayosaidia maafisa hao kuwafikia wananchi hadi ngazi ya chini.

“Tumekuwa tukinunua magari kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa maafisa kilimo katika maeneo mbalimbali nchini. Hata juzi tumepokea magari mengine na tutaangalia utaratibu wa kuyapeleka katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ikiwemo Arumeru Magharibi,” alisema Silinde.

Naibu Waziri huyo aliwahakikishia wananchi wa Arumeru Magharibi kuwa Serikali inalifahamu tatizo hilo na itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa maafisa kilimo ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa wakulima.

Post a Comment

Previous Post Next Post