DKT. LUKUMAY APIGANIA MAENDELEO YA WANANCHI WA ARUMERU MAGHARIBI ATETA NA WAZIRI CHANDE BUNGENI

 DKT. LUKUMAY APIGANIA MAENDELEO YA WANANCHI WA ARUMERU MAGHARIBI

Joseph Ngilisho-Arushadigital – DODOMA

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Johannes Lembulung Lukumay ameendelea kuonyesha juhudi kubwa za kuwatumikia wananchi wa jimbo lake baada ya kuiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza msaada wa miradi ya maendeleo kwa kata na vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Msitu wa Meru-USA pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Arusha.

Dkt. Lukumay alitoa ombi hilo bungeni wakati akichangia hoja mbele ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, ambapo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ujirani mwema kati ya hifadhi hizo na wananchi wanaozunguka maeneo hayo.

Alisema wananchi wanaoishi karibu na hifadhi wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika uhifadhi wa rasilimali za taifa, hivyo kuna haja ya Serikali kuona namna bora ya kurudisha faida kwa jamii kupitia utekelezaji wa miradi ya huduma za kijamii ikiwemo maji safi na salama, elimu, afya pamoja na miundombinu ya barabara.

Dkt. Lukumay alieleza kuwa baadhi ya vijiji vinavyopakana na hifadhi hizo bado vinakabiliwa na changamoto mbalimbali za maendeleo, hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi za uhifadhi na wananchi.

Katika hoja yake, mbunge huyo aliainisha kata na vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Msitu wa Meru-USA ambavyo vinahitaji kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kuwa ni Kata ya Oldonyowas yenye vijiji vya Losinoni Chini, Losinoni Juu na Engutukoit.

Pia alitaja Kata ya Oldonyosambu yenye vijiji vya Oldonyosambu, Lemanda na Lemong’o, huku Kata ya Olmotonyi ikitajwa kuwa na vijiji vya Olmotonyi, Ngaramtoni na Emaoi vinavyohitaji kuboreshwa huduma za kijamii.

Aidha, alieleza kuwa Kata ya Kimunyak yenye vijiji vya Kimunyak na Olmuringaringa, Kata ya Kiutu kupitia kijiji cha Olgilai, pamoja na Kata ya Sambasha yenye vijiji vya Timbolo na Sambasha nayo inapaswa kunufaika na miradi hiyo.

Mbali na hayo, Dkt. Lukumay alitaja Kata ya Olturoto kupitia kijiji cha Oldonyosapuk, Kata ya Soon II kupitia kijiji cha Ng’iresi, pamoja na Kata ya Bangata yenye vijiji vya Midawe na Sasi kuwa sehemu muhimu zinazohitaji kuimarishiwa huduma za maendeleo kutokana na ukaribu wake na maeneo ya hifadhi.

Kwa upande wa vijiji vinavyopakana na Arusha National Park, mbunge huyo alitaja Kata ya Bangata yenye vijiji vya Midawe na Sasi, Kata ya Oldonyowas yenye vijiji vya Engutukoit na Lesinoni Juu, pamoja na Kata ya Oldonyosambu kupitia vijiji vya Lemong’o na Lemanda.

Dkt. Lukumay alisema kuwa kuimarishwa kwa huduma za maji, afya, elimu na barabara katika maeneo hayo kutasaidia kuongeza ushirikiano kati ya wananchi na mamlaka za hifadhi, sambamba na kulinda mazingira na rasilimali za taifa.

Alisisitiza kuwa wananchi wanaozunguka hifadhi wanapaswa kuona manufaa ya moja kwa moja yatokanayo na uwepo wa hifadhi hizo ili kuendelea kuwa walinzi wa kwanza wa uhifadhi na utalii nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Hassan Chande, aliahidi kuyafanyia kazi maeneo yote yaliyowasilishwa na mbunge huyo kwa kushirikiana na taasisi husika chini ya wizara hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi wanaendelea kunufaika na rasilimali za taifa.

Ends

Post a Comment

0 Comments