MOTO WATEKETEZA JENGO LA MAHAKAMA CHALINZE, NYARAKA MUHIMU ZATEKETEA

 MOTO WATEKETEZA JENGO LA MAHAKAMA CHALINZE, NYARAKA MUHIMU ZATEKETEA

Na ArushaDigital | PWANI

Jengo la Mahakama ya Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani limeteketea kwa moto mkubwa uliotokea usiku wa kuamkia leo, Aprili 7, mwaka huu, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali pamoja na kuteketea kwa nyaraka mbalimbali muhimu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salum Morcase, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa moto huo ulianza majira ya saa 8:30 usiku na kuenea kwa kasi, hali iliyosababisha jengo lote kuteketea kabla ya kudhibitiwa.

Amesema mara baada ya kupokea taarifa za tukio hilo, vikosi vya Polisi kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) walifika eneo la tukio na kuanza juhudi za kuuzima moto huo.

“Chanzo cha moto bado hakijafahamika, na tathmini ya awali ya thamani ya mali zilizoharibiwa inaendelea kufanyika. Hadi sasa, hakuna madhara ya kibinadamu yaliyoripotiwa,” alisema Kamanda Morcase.

Kwa mujibu wa taarifa za awali, moto huo unadaiwa kuanza katika moja ya vyumba vya jengo hilo kabla ya kusambaa kwa haraka na kuathiri sehemu kubwa ya mahakama hiyo.

Polisi mkoani Pwani wamewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia katika uchunguzi wa tukio hilo, huku wakisisitiza umuhimu wa taasisi za umma na binafsi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo ya usalama wa majengo yao ili kuzuia majanga kama hayo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Tonga, ambako mahakama hiyo ipo, Mathias Paulo, alisema kuwa tukio hilo liligunduliwa na mmoja wa wakazi jirani aliyebaini moto ukianza kutoka katika moja ya vyumba vya jengo hilo.

“Baada ya kuona moshi na moto, alitoa taarifa haraka kwa viongozi wa kijiji, ambao nao waliwasiliana na vyombo vya usalama. Hata hivyo, kufikia wakati vikosi vya zimamoto vinafika, moto ulikuwa tayari umesambaa na kusababisha uharibifu mkubwa,” alisema Mathias.

Tukio hilo limeibua wasiwasi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, hususan kutokana na umuhimu wa jengo hilo katika utoaji wa huduma za haki kwa wananchi, pamoja na upotevu wa nyaraka ambazo zinaweza kuathiri mwenendo wa mashauri mbalimbali.

Uchunguzi wa kina unaendelea kubaini chanzo halisi cha moto huo pamoja na hasara kamili iliyosababishwa.

Ends...

Post a Comment

0 Comments