MNYIKA AAGIZA OFISI ZA CHADEMA NCHI NZIMA ZIFUNGULIWE RASMI BAADA YA ZUIO KUONDOLEWA NA MAHAKAMA YA RUFAA

 CHADEMA YAFUNGUA RASMI OFISI ZAKE NCHI NZIMA BAADA YA ZUIO KUONDOLEWA NA MAHAKAMA YA RUFAA

Na Arusha Digital | Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, ametangaza rasmi kufunguliwa kwa ofisi zote za chama hicho kuanzia leo Aprili 15, 2026, kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania kuondoa zuio lililokuwa likikizuia chama hicho kufanya shughuli zake za kisiasa na kiutendaji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, Mnyika amesema hatua hiyo inaashiria kurejea rasmi kwa shughuli za kawaida za chama baada ya kipindi kirefu cha kusitishwa kwa shughuli hizo.

Amesema huu ni mkutano wa kwanza kufanyika katika ukumbi wa makao makuu ya CHADEMA tangu kutolewa kwa zuio la Mahakama mnamo Juni 10, 2025, akieleza kuwa kwa zaidi ya siku 310 ofisi hizo zilikuwa zimefungwa.

“Ndugu wanahabari, tunawashukuru kwa kuitikia wito wetu wa dharura. Leo ni siku ya kihistoria kwani ni mara ya kwanza tangu kutolewa kwa zuio la Mahakama, ukumbi huu unafunguliwa rasmi na tunafanya mkutano na wanahabari,” amesema Mnyika.

Mnyika amedai kuwa licha ya chama hicho kuona amri hiyo ya zuio kuwa haikuwa halali na haikuhusu viongozi wote, waliamua kuheshimu utawala wa sheria kwa kusitisha shughuli za kiutendaji ili kuepusha mvutano zaidi na mamlaka za dola.

Ameeleza kuwa hata baada ya muda wa miezi sita wa zuio hilo kumalizika Desemba 10, 2025, bado kulikuwepo na utekelezaji wa amri hiyo, hali aliyodai iliendelea kukwamisha shughuli za chama.

“Sisi kama chama kinachoheshimu misingi ya utawala wa sheria hatukutaka kutoa mwanya wa visingizio kwa mamlaka, hivyo tuliamua kufunga ofisi zetu kwa shughuli za kiutendaji hadi hapo haki itakapopatikana,” ameongeza.

Kutokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, Mnyika ametangaza kuwa ofisi za makao makuu zimefunguliwa rasmi na kuanza kufanya kazi mara moja, huku akitoa wito kwa viongozi wa chama katika ngazi zote kuhakikisha ofisi za chama zinafunguliwa kote nchini.

Amesisitiza kuwa kuanzia sasa, shughuli zote za kiofisi, uratibu na mipango ya chama zinapaswa kuendelea kama kawaida katika mikoa na wilaya zote.

“Kwa mamlaka niliyopewa kama Mtendaji Mkuu wa Chama, natangaza rasmi kuwa ofisi za makao makuu zimefunguliwa na kazi zinaendelea mara moja. Viongozi wetu kote nchini wahakikishe wanafungua ofisi na kuanza kazi bila kusita,” amesema.

Hatua hiyo inatajwa kuwa mwanzo mpya kwa CHADEMA katika kuimarisha shughuli zake za kisiasa na kiutendaji, baada ya kipindi cha zaidi ya miezi kumi cha changamoto za kisheria zilizokuwa zikikikabili chama hicho.

Post a Comment

0 Comments