LATRA YAPIGA MARUFUKU UPANDISHAJI HOLELA WA NAULI, YATAKA UTARATIBU UFUATWE

  LATRA YAPIGA MARUFUKU UPANDISHAJI HOLELA WA NAULI, YATAKA UTARATIBU UFUATWE

Na Arusha Digital



Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini nchini, LATRA, imewataka wadau wote wa sekta ya usafirishaji kujizuia kupandisha nauli kiholela kwa kisingizio cha kupanda kwa bei za mafuta, ikisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka utaratibu uliowekwa.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Dkt. Habibu Suluo, alisema mamlaka hiyo haitavumilia vitendo vya baadhi ya wasafirishaji wanaotumia mabadiliko ya gharama za mafuta kama kigezo cha kuongeza nauli bila kufuata taratibu rasmi.


Alisema kuwa LATRA imepanga kufanya kikao muhimu cha wadau wa sekta ya usafirishaji tarehe 8 Aprili jijini Dar es Salaam, ambapo hoja ya mabadiliko ya nauli itajadiliwa kwa kina kwa kuzingatia hali halisi ya soko na maslahi ya wananchi.


“Tunatambua changamoto ya kupanda kwa bei za mafuta, lakini ni muhimu wadau wakafuata utaratibu uliowekwa. Hakuna ruhusa ya kupandisha nauli kiholela bila idhini ya mamlaka husika,” alisisitiza Dkt. Suluo.


Aidha, aliwataka watoa huduma za usafirishaji kuwa na uelewa wa hali ngumu ya maisha kwa wananchi, akibainisha kuwa ongezeko la gharama za maisha tayari linaathiri watumiaji wa huduma hizo.


“Wananchi nao wanaumizwa na hali hii, hivyo ni vyema wasafirishaji wakaonesha uwajibikaji na huruma badala ya kukimbilia kuongeza nauli bila kufuata sheria,” aliongeza.


Katika hatua nyingine, LATRA imewataka wasafirishaji wote wenye nia ya kupandisha nauli kuwasilisha maombi yao rasmi yakifafanua sababu, kiwango kinachopendekezwa na athari zake, ili mamlaka iweze kuyapitia na kutoa maamuzi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.


Tamko hilo linakuja wakati kukiwa na malalamiko kutoka kwa abiria katika maeneo mbalimbali nchini kuhusu baadhi ya watoa huduma kupandisha nauli bila ridhaa ya mamlaka, hali inayozua sintofahamu na mzigo kwa watumiaji wa huduma za usafiri.




Ends..

Post a Comment

0 Comments