MAMLAKA YAKAMATA KILO 106 ZA MIRUNGI LONGIDO, DIWANI ANASWA
Na Joseph Ngilishi | Arushadigital
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imefanikiwa kukamata kilo 106.25 za dawa za kulevya aina ya mirungi katika Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, zikiwa zinasafirishwa kwa gari aina ya Toyota Wish lenye namba ya usajili T 889 DPG.
Diwani wa Kimokouwa, Solomon KoholoAkizungumza na waandishi wa habari Aprili 14, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo, amesema kuwa katika tukio hilo watu wawili wanashikiliwa na vyombo vya dola kwa tuhuma za kuhusika na usafirishaji wa dawa hizo.
Ametaja watuhumiwa hao kuwa ni Diwani wa Kata ya Kimokouwa, Solomon Koholo (38), pamoja na Lekaneti Kukuu (38).
Lyimo amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni sehemu ya operesheni endelevu za mamlaka hiyo za kukabiliana na biashara ya dawa za kulevya nchini, akionya kuwa hakuna mtu atakayevumiliwa kujihusisha na vitendo hivyo bila kujali umaarufu wake.
“Tumebaini kuwepo kwa mtandao unaojumuisha watu mbalimbali, wakiwemo baadhi ya watu maarufu, wanaotumika kwa namna moja au nyingine katika biashara hii haramu. Tunatoa onyo kali kuwa tutamchukulia hatua yeyote atakayebainika kuhusika,” amesema Lyimo.
Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imeripoti kukamata kilo 68.3 za mirungi katika maeneo ya Himo na Same mkoani Kilimanjaro, ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa.
Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Amin Mazua (58), maarufu kwa jina la Mbaruku, pamoja na Wilbard Mchau (50).
Aidha, Lyimo amesema kuwa operesheni hizo zimefanikisha pia kukamatwa kwa aina nyingine za dawa za kulevya katika maeneo mbalimbali nchini, huku akisisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa hizo yanaendelea kwa nguvu zote.
Amesema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha biashara ya dawa za kulevya inatokomezwa kabisa nchini.


0 Comments