SERIKALI YATIA SAINI MIRADI YA BARABARA ZA AFCON 2027 ARUSHA KWA BILIONI 81.5

 SERIKALI YATIA SAINI MIRADI YA BARABARA ZA AFCON 2027 ARUSHA KWA BILIONI 81.5

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA


SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI imecihukua hatua kubwa ya kimkakati katika maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya AFCON 2027, baada ya kutia saini mikataba ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya barabara katika Jiji la Arusha, hatua inayotarajiwa kuibadilisha sura ya jiji hilo kiuchumi na kijamii.

Akiongoza hafla hiyo leo Machi 20, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, alisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa viwango vya kimataifa, huku ikiimarisha miundombinu ya ndani kwa manufaa ya muda mrefu.

Mradi huo mkubwa unahusisha ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa jumla ya kilometa 13.4, zikijumuisha kipande cha Mateves–Bondeni (Km 6.5), Lendita (Km 2.75) pamoja na Esuri (Km 2.45). Baadhi ya barabara hizo zitajengwa kwa njia nne (dual carriageways), hatua itakayopunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa usafiri jijini humo.

Kwa mujibu wa Waziri Shemdoe, mradi huo unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 81.5, ukifadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania, na unatarajiwa kukamilika kabla ya kuanza kwa mashindano ya AFCON 2027.

“Hatuna nafasi ya kuchelewa. Huu ni mradi wa kimkakati unaobeba taswira ya nchi yetu kimataifa. Wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa weledi, kasi na ubora wa hali ya juu bila kuongeza muda wa utekelezaji,” alisisitiza Waziri Shemdoe.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Arusha alieleza kuwa mkoa huo umebahatika kupata fursa adhimu ya kuwa sehemu ya maandalizi ya mashindano hayo makubwa barani Afrika, akibainisha kuwa ushirikiano wa wananchi utakuwa nguzo muhimu katika kufanikisha miradi hiyo kwa wakati.

Aidha, alitoa wito kwa wakazi wa Arusha kushiriki kikamilifu katika kulinda na kusimamia miradi hiyo ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana na miundombinu hiyo inadumu kwa muda mrefu.

Wachambuzi wa maendeleo wanaeleza kuwa uwekezaji huo si tu utaiwezesha Tanzania kuandaa mashindano ya AFCON 2027 kwa mafanikio, bali pia utafungua fursa mpya za kiuchumi, ikiwemo kukuza sekta ya utalii, biashara na ajira, huku Jiji la Arusha likitarajiwa kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na ongezeko la wageni wa kimataifa.

Mradi huu unatajwa kuwa kichocheo kipya cha mageuzi ya miundombinu ya mijini, ukiweka msingi imara wa maendeleo endelevu na kuifanya Arusha kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kimataifa nchini.













Ends..

Post a Comment

0 Comments