MWALIMU ACHINJWA KIKATILI KATAVI, MWILI WATUPWA NJIANI
Na Arushadigital |KARAVI
Tahadhari na hofu vimetanda miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi kufuatia tukio la kusikitisha la kuuawa kikatili kwa mwalimu wa Shule ya Msingi Nguvumali, aliyefahamika kwa jina la Aidan Ramadhani (42-43), ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa umetenganishwa kichwa na kiwiliwili.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, mwalimu huyo aliuawa usiku wa kuamkia Machi 20, 2026, ambapo watu wasiojulikana walimtekelezea mauaji hayo ya kinyama kabla ya kuutelekeza mwili wake katikati ya Mtaa wa Mkwajuni, Kata ya Mwamkulu, katika Manispaa ya Mpanda.
Wananchi wa eneo hilo walikumbwa na taharuki kubwa walipouona mwili huo asubuhi, hali iliyozua simanzi, hofu na maswali mengi kuhusu usalama wa raia katika eneo hilo. Baadhi ya wakazi wamesema tukio hilo ni la kinyama na halijawahi kushuhudiwa kwa muda mrefu katika mtaa huo.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkwajuni, Amos Mkingwa, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa limewaacha wananchi katika hali ya mshangao na majonzi makubwa.
Amesema kuwa mauaji hayo ni ya kikatili na yasiyo ya kawaida, huku akitoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na vyombo vya dola ili kusaidia kufichua waliohusika na tukio hilo.
“Ni tukio la kusikitisha sana na limetuumiza kama jamii. Tunaomba wananchi watoe taarifa zozote zitakazosaidia kubaini wahusika ili sheria ichukue mkondo wake,” amesema Mkingwa.
Kwa sasa, vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo pamoja na kuwakamata wahusika, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika hospitali ya Mkoa wa Katavi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Tukio hilo linaibua upya mjadala kuhusu usalama wa raia na umuhimu wa jamii kushirikiana na mamlaka husika katika kuzuia vitendo vya uhalifu vinavyozidi kushika kasi katika baadhi ya maeneo nchini.
Ends...

0 Comments