MAFURIKO YAHARIBU SHULE YA MSINGI ENGARUKA JUU MONDULI
Na Joseph Ngilisho | MONDULI
MWENYEKITI wa Baraza la Shule Wilaya ya Monduli, Mheshimiwa Kisoki Mwaetiko, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuhamisha Shule ya Msingi Engaruka Juu iliyopo katika Kata ya Engaruka, baada ya mafuriko makubwa kuharibu miundombinu yake kufuatia mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Machi 9, 2026.
Mwaetiko ametoa wito huo baada ya kutembelea shule hiyo na kujionea uharibifu mkubwa uliosababishwa na mafuriko hayo, akisema eneo ilipojengwa shule hiyo liko katika mkondo wa maji jambo linaloifanya iwe katika hatari ya kukumbwa na maafa ya mara kwa mara.
“Shule hii ipo katika porongo la maji. Tunaiomba Serikali iangalie namna ya kuiondoa katika eneo hili ili wanafunzi waweze kusoma katika mazingira salama na yenye amani,” amesema.
Mafuriko hayo yalisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya shule hiyo, hali iliyolazimisha kusitishwa kwa muda kwa shughuli za masomo ili kupisha tathmini ya kina ya madhara yaliyotokea.
Baadhi ya athari zilizoripotiwa ni pamoja na mabweni ya wanafunzi kujaa tope, kubomoka kwa ukuta wa shule wenye urefu wa takribani mita 100, kuvunjika kwa milango yenye nondo za ulinzi pamoja na baadhi ya vifaa vya wanafunzi kusombwa na maji.
Aidha, mafuriko hayo yameharibu samani na vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo vitanda 35, magodoro 75 pamoja na maktaba ya vitabu ambayo ilijaa tope na kuharibu vitabu vingi.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwaetiko amesema hali aliyojionea inaonesha ukubwa wa maafa yaliyotokea, huku akishukuru kwamba wanafunzi wote waliokuwepo shuleni hapo waliweza kuokolewa salama.
“Kwa kweli tukio hili ni kubwa sana, lakini tunashukuru Mungu kwamba hakuna mwanafunzi aliyepoteza maisha. Walimu pamoja na viongozi wa kijiji walifanya kazi kubwa kuhakikisha wanafunzi wote wanatolewa katika maeneo hatarishi na kufikishwa salama kwa wazazi na walezi wao,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Engaruka Juu, Bw. Meimute, amemshukuru Mwenyekiti wa Baraza la Shule pamoja na viongozi wengine wa wilaya kwa kufika shuleni hapo na kujionea hali halisi ya uharibifu uliotokea.
Amesema kwa sasa uongozi wa shule kwa kushirikiana na jamii unaendelea na juhudi za kuokota baadhi ya vifaa na mali za wanafunzi zilizochukuliwa na mafuriko hayo.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo aliambatana na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Sepeko, pamoja na Diwani wa Kata ya Engaruka, Mheshimiwa Onesmo Nakoyo.
Akizungumzia tukio hilo, Nakoyo amesema shule hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi takribani 1,500, lakini kufikia Alhamisi wanafunzi wote walikuwa tayari wameondolewa katika eneo hilo hatarishi na kurudishwa kwa wazazi wao kutokana na hali mbaya ya mazingira iliyosababishwa na mafuriko.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Engaruka, Abraham Legolia, ameomba Serikali ichukue hatua za haraka kulishughulikia suala hilo, akieleza kuwa kutokana na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo, shule hiyo ipo katika mkondo wa maji na huathiriwa kila mvua kubwa inaponyesha.
“Hali ya kijiografia ya eneo hili inaifanya shule kukumbwa na mafuriko mara kwa mara. Tunaomba Serikali iangalie suluhisho la kudumu ili kulinda maisha ya wanafunzi na mali za shule,” amesema.
Kwa sasa shule hiyo imefungwa kwa muda kupisha tathmini ya athari zilizotokea na hatua za kurejesha miundombinu iliyoharibika.
Ends..



0 Comments