DC KARANGA AKANUSHA VIKALI TAARIFA ZA MAFURIKO NA VIFO KARATU,AWASHUTUMU VIKALI WANDISHI KWA UPOTOSHAJI ADAI WAMEJITENGA NA MAADILI ,ASISITIZA KARATU NI SALAMA KWA UTALII

DC Karatu Lameck Karanga Akanusha Vikali Taarifa za Mafuriko, Awashutumu Waandishi kwa Upotoshaji

Na Joseph Ngilisho | ARUSHA

MKUU wa Wilaya ya Karatu, Lameck Karanga, amekanusha vikali taarifa zinazosambazwa kuhusu kuwepo kwa mafuriko makubwa wilayani humo, akizitaja kuwa ni za uongo na zenye lengo la kupotosha umma pamoja na kuleta taharuki isiyo ya lazima.

Akizungumza kuhusu hali halisi ya wilaya hiyo, Karanga alisema kuwa hakuna madhara makubwa yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha, huku akisisitiza kuwa hakuna vifo wala nyumba zilizozama kama inavyodaiwa katika taarifa hizo.

Alieleza kuwa serikali ya wilaya imefanya tathmini ya kina kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa, madiwani pamoja na kamati za maafa, na kubaini kuwa hali iko shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kawaida bila athari kubwa.

Akifafanua zaidi, DC Karanga alikiri kuwepo kwa bwawa linalokusanya maji wilayani humo, lakini akasisitiza kuwa halijasababisha madhara yoyote kwa wananchi.

“Ni kweli kabisa Karatu tunalo bwawa ambalo hujaa maji hasa kipindi hiki cha mvua, lakini taarifa zinazosambazwa kwamba kuna nyumba zaidi ya 20 zimezama na watu wamepoteza maisha ni uongo mkubwa. Hakuna kitu kama hicho,” alisisitiza.

Aliongeza kuwa hadi sasa hakuna nyumba iliyozama kwenye maji wala tukio lolote la vifo lililoripotiwa, akishangazwa na namna taarifa hizo zilivyosambazwa bila kuthibitishwa.

“Hata mimi kama Mkuu wa Wilaya hawakuniuliza ili kupata ufafanuzi kabla ya kutoa taarifa hiyo. Hii inaonesha wazi kutokuwapo kwa weledi na kutokuzingatia misingi ya taaluma ya uandishi wa habari,” alisema.

Katika hatua nyingine, DC Karanga aliwashutumu baadhi ya waandishi wa habari kutoka kituo kimoja cha redio wilayani humo kwa kusambaza taarifa hizo bila kufanya uchunguzi wa kutosha, akidai kuwa wamekiuka misingi ya taaluma ya uandishi wa habari.

Alieleza kuwa kati ya waandishi wawili wanaotuhumiwa kusambaza taarifa hizo za uongo, mmoja wao amekuwa na tabia ya mara kwa mara ya kuchafua taswira ya wilaya hiyo kwa kuandika habari zisizo na ukweli.

“Si mara ya kwanza kwa mwandishi huyu kuleta taharuki hapa Karatu. Amekuwa akiandika taarifa zisizo sahihi ambazo mara kadhaa zimezua hofu kwa wananchi. Inaonekana wazi amepuuza au kupoteza kabisa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari,” alisema.

Aliongeza kuwa changamoto kubwa kwa mwandishi huyo ni kushindwa kuzingatia misingi ya mizania ya habari kwa kutotoa nafasi kwa upande wa serikali kueleza ukweli kabla ya kuchapisha au kurusha taarifa.

“Habari lazima iwe na pande zote. Huwezi kuripoti jambo kubwa kama hili bila kuzungumza na mamlaka husika. Kutofanya hivyo ni upotoshaji wa makusudi,” alisisitiza.

Alionya kuwa tabia ya kusambaza taarifa zisizothibitishwa inaweza kuathiri amani ya jamii pamoja na sekta muhimu za uchumi, hususan utalii unaotegemewa katika maeneo ya Karatu, Ngorongoro na Serengeti.

Aidha, alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa taarifa sahihi kwa wakati na kuwataka waandishi wa habari kuzingatia weledi, maadili na wajibu wao wa kuhakikisha wanatoa habari zilizo sahihi na zenye mizania.

Alimalizia kwa kuwahakikishia wananchi kuwa Wilaya ya Karatu ipo salama, huku akiwataka kupuuza taarifa za uzushi na kuendelea na shughuli zao kwa utulivu.

Awali waandishi wawili Wolter Mbaga na Nobert Hongoli wa kituo binafsi cha radio wilayani humo, walidaiwa kukamatwa na kuwekwa mahabausu kwa kosa la kutoa taarifa za upotoshaji juu ya athari ya mafuriko ya mvua walizodai yamezamisha nyumba 20 na madai ya watu kufa maji.

Dc alisisitiz kwa kuwataka waandishi wa habari kuzingatia maadili ya taaluma yao kwa kujitenga na taarifa za uongo ,uchochezi,uchonganishi na upotoshaji ,akidai ni vema kuzitafuta mamlaka husika kwa ajili ya ufafanuzi kabla ya kuzipeleka hewani.


Picha za bwawa la maji wilayani Karatu,linalodaiwa kujaa maji na kuzamisha nyumba zaidi ya 20.DC amekanusha vikali akidai ni upotoshaji .

Ends..

Post a Comment

0 Comments