WEZI WA AMBULANCE YA WAGONJWA WAKAMATWA ARUSHA WAKIWA WAMELIBADI KUWA GARI LA UTALII
Na Joseph Ngilisho – MARA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Rutumo, alisema Jeshi la Polisi limepata mafanikio makubwa baada ya kuwakamata watuhumiwa wanne waliodaiwa kuiba gari la serikali aina ya Land Cruiser, namba za usajili STM 7830, mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lililokuwa likitumika kama gari la kubebea wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Rutumo alisema gari hilo liliibiwa katika mazingira ya utata likiwa limeegeshwa katika ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, kabla ya wahalifu hao kuliondoa na kulisafirisha hadi jijini Arusha.
Alisema baada ya kulifikisha Arusha, watuhumiwa hao waliliingiza gari hilo katika garage bubu, ambako lilifanyiwa mabadiliko makubwa ya mwonekano na matumizi kwa kuligeuza kuwa gari la utalii, kwa lengo la kuficha uhalisia wake na kulipotosha Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Rutumo, operesheni ya kuwanasa watuhumiwa hao ilifanyika kwa weledi wa hali ya juu, uaminifu na ushirikiano mkubwa kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wema, hali iliyowezesha kufanikisha kazi hiyo nyeti.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Goodluck Steven Chata (28) mkazi wa Tarime mjini; Karume Kimweri (64) mkazi wa Mrombo jijini Arusha; Said Husein Ramadhani (39) mkazi wa Arusha pamoja na Eriya Joakim Mulimo (23) naye mkazi wa Arusha.
Kamanda Rutumo ameongeza kuwa baada ya kukamatwa, watuhumiwa hao walisafirishwa kutoka Arusha hadi Musoma kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiwa umekamilika.
Alisema taratibu za mwisho zinaendelea na kwamba watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani wakati wowote ili kujibu tuhuma zinazowakabili, huku Jeshi la Polisi likiendelea na juhudi za kubaini iwapo kuna watu wengine waliokuwa wanahusishwa na uhalifu huo.
Kamanda huyo amewapongeza wananchi kwa kutoa taarifa muhimu zilizosaidia kufanikisha operesheni hiyo, na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali dhidi ya watu wote wanaojihusisha na wizi wa mali za umma, hususan mali zinazohusiana moja kwa moja na huduma za kijamii kama afya.
Ends.....



0 Comments