KAULI YA WAZIRI MKUU YABEBWA MBELE: ELIMU YA PEMBEZONI NI MSINGI WA MAENDELEO
SERIKALI YASISITIZA MIUNDOMBINU YA ELIMU LONGIDO, YAWEKA JIWE LA MSINGI SHULE YA SEKONDARI SINYA
Na Joseph Ngilisho – LONGIDO
WAZIRI Mkuu Mwigulu Nchemba ametoa kauli nzito ya serikali kuhusu vipaumbele vya elimu vijijini, akisisitiza utekelezaji wa haraka wa miradi ya miundombinu katika halmashauri ya Longido huku akiweka jiwe la msingi la ujenzi katika Shule ya Sekondari Sinya na kuipongeza halmashauri hiyo kwa kusamaianva miradi hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi na mradi wa maji, Waziri Mkuu alieleza kuwa uwekezaji katika makazi ya walimu, mabweni ya wanafunzi na huduma ya maji safi ni sharti la kuinua kiwango cha elimu, hasa katika maeneo ya pembezoni.
“Miundombinu ya makazi ya walimu na mabweni katika eneo hili ni lazima ikamilike. Mazingira bora ya kujifunzia ndiyo msingi wa mafanikio ya wanafunzi na maendeleo ya taifa,” alisisitiza.
Alielekeza viongozi wa serikali za mitaa, TAMISEMI na wadau wa elimu kuhakikisha changamoto zilizobainishwa zinapatiwa ufumbuzi wa haraka, akisisitiza kuwa serikali haitavumilia ucheleweshaji wa miradi ya kijamii.
Katika kuimarisha huduma za maji, Waziri Mkuu alinukuu maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba maeneo yenye changamoto ya maji, hususan yale yenye shughuli za kiuchumi kama uchimbaji, yanapaswa kupewa kipaumbele katika miradi ya maji vijijini ili wananchi wanufaike moja kwa moja na rasilimali zao.
Alibainisha kuwa ushiriki wa wananchi wa Sinya kupitia michango ya vifaa vya ujenzi uliharakisha utekelezaji wa miradi na kupunguza gharama, akisisitiza kuwa mshikamano huo ni mfano wa mafanikio ya ushirikiano kati ya serikali na jamii.
Hata hivyo, aliomba serikali kuendelea kusaidia ujenzi wa nyumba zaidi za walimu, mabweni na uzio wa shule kutokana na uwepo wa wanyama wakali katika mazingira yanayoizunguka.
Waziri Mkuu alisisitiza kuwa mapato ya taifa, hususan kutoka sekta ya madini, yanaendelea kuelekezwa katika miradi ya elimu, afya na maji ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi moja kwa moja. Alibainisha kuwa katika miaka minne iliyopita serikali imejenga shule za sekondari za wasichana katika kila mkoa, shule maalum za wavulana katika kanda mbalimbali na hospitali za wilaya pamoja na maelfu ya madarasa nchini.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa wito kwa viongozi wa eneo hilo kuimarisha ushirikiano katika usimamizi wa miradi ya maendeleo ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.
Uwekaji wa jiwe la msingi Shule ya Sekondari Sinya umeonekana kuwa alama mpya ya matumaini kwa wananchi wa Longido, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za elimu na kuchochea maendeleo ya kijamii katika eneo hilo la mpakani.
Wakati huo huo Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemb alitembelea na kukagua maendeleo ya Mradi wa Majisafi wa Sinya–Namanga unaotekelezwa kwenye Kijiji cha Sinya, wilaya ya Longido
Kupitia mradi huo, Dkt Mwigulu alimpongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza mradi huo ambao ilikuwa ni kilio cha wananchi wa Longido ambacho walikiwakilisha wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwaka 2025.
"Kufuatia changamoto hiyo ya maji, Mhe. Rais aliagiza watalamu kwenda Longido kutafuta maji kwa gharama yoyote ili wananchi na mifugo yao waweze kuoata huduma hiso"Alisema
Hata hivyo, akisoma taarifa ya mradi huo Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira Arusha -AUWSA, Mhandisi Rujomba, amesema kuwa mradi huo, natekelezwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 13.5, mradi unatekelezwa na Mkandarasi M/s. Zongii Contractors Co. Ltd,
Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uzalishaji wa maji kufikia Lita 4,100,000 kwa siku ili kukidhi mahitaji ya wananchi na mifugo, mradi unafanyika kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa Sinya na Mji wa Namanga, kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya maji ambayo chanzo cha sasa cha Mto Simba ambacho hakitoshelezi.
Awali, Waziri Mkuu yuko wilaya ya Longido, ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Mkoani Arusha.
Ends .








0 Comments