Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo jijini Arusha, hususan ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Bondeni City Bus Terminal na Soko la Kilombero, akisisitiza uwajibikaji, matumizi sahihi ya fedha za umma na uboreshaji wa mazingira ya biashara kwa wananchi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara leo february 24,2026 uliofanyika eneo la Soko la Kilombero, Waziri Mkuu alisema kukamilika kwa stendi mpya ya mabasi inayojengwa katika kata ya Murieth kutapunguza msongamano uliopo sasa, kupanua huduma za usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi jijini humo.
“Stendi ya sasa ni finyu na imebana sana. Mradi huu mpya utaongeza nafasi, kuboresha huduma na kufungua fursa zaidi za kibiashara kwa wananchi,” alisema.
Katika kuimarisha miundombinu ya jiji, Dkt. Nchemba alielekeza baadhi ya barabara muhimu zijengwe kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa pamoja na kuongeza ufanisi wa huduma za usafiri wa mijini.
Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji, John Kayombo, kuongeza idadi ya masoko rasmi ili kuwapa wafanyabiashara maeneo bora, salama na yenye wateja wa uhakika.
Alisisitiza kuwa soko jipya la Kilombero litawapa kipaumbele wafanyabiashara waliopisha eneo la mradi huo, huku akionya vikali vitendo vya ulanguzi, wizi na upendeleo katika ugawaji wa maduka.
“Nataka haki itendeke. Fanyeni sensa kubaini wahusika halali. Mtumishi wa umma atakayebainika kujimilikisha duka kinyume cha utaratibu atachukuliwa hatua kali,” alisisitiza.
Aidha, alielekeza masoko yote yawe safi, salama na yaendeshwe kwa mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu, kudhibiti udanganyifu na kulinda mali za wafanyabiashara.
Baada ya mkutano huo, Waziri Mkuu alipokea na kusikiliza kero za wananchi mmoja mmoja na kutoa maelekezo ya papo kwa papo kwa viongozi wa jiji ili kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.
Miradi ya Kimkakati ya Jiji
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa Jiji alisema ziara ya Waziri Mkuu ni motisha kwa wafanyabiashara na jamii kwa ujumla, ikionyesha dhamira ya serikali kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi.
Kituo cha Mabasi cha Bondeni City kinajengwa kwa miundombinu ya kisasa ikiwemo maegesho ya magari makubwa na madogo, maeneo ya kupakia na kushusha abiria, mifumo ya usalama na huduma za mizigo.
Mradi huo unatarajiwa kurahisisha usafiri wa abiria wanaosafiri ndani na nje ya nchi jirani pamoja na kupunguza msongamano katikati ya jiji.
Soko la Kilombero ni sehemu ya miradi minne inayotekelezwa chini ya mpango wa TACTIC kwa ufadhili wa Benki ya Dunia. Mradi unahusisha uboreshaji wa mazingira, mifumo ya maji ya mvua na maji taka, maegesho ya magari na miundombinu rafiki kwa watu wote, wakiwemo wenye ulemavu.
Soko hilo limepangwa kwa viwango vya kisasa likiwa na Vizimba 518 vinavyoweza kuhudumia wafanyabiashara 2,072 kwa wakati mmoja,Maliwato ya kisasa kwa jinsia zote na kwa wazee na wenye ulemavu
Pia soko hilo lina Kituo cha polisi, ofisi ya zimamoto na chumba cha huduma ya kwanza Bustani ya mapumziko na maegesho rasmi ya magari, malori, boda boda na bajaji
Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Mohammedi Builders Limited kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.5. Ulianza Mei 30, 2025 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, 2026. Hadi sasa umefikia asilimia 66 ya utekelezaji, huku mkandarasi akilipwa Shilingi bilioni 3.95 sawa na asilimia 41.66 ya gharama ya mradi.
Faida za Kijamii na Kiuchumi
Mradi wa soko unatarajiwa kuongeza ajira, mapato ya wafanyabiashara na mapato ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Pia utaimarisha huduma za kifedha, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji kwa kuwepo maegesho rasmi ya vyombo vya usafiri.
Pamoja na changamoto ya upatikanaji wa baadhi ya vifaa wakati wa uchaguzi mkuu iliyosababisha ucheleweshaji wa asilimia 5.5, mkandarasi ameongeza zamu za usiku ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huo, pamoja na ziara ya Waziri Mkuu iliyolenga kuimarisha usimamizi na kasi ya maendeleo ya jiji.
Ends..








0 Comments