Na Arushadigital – Biharamulo
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Simon Sirro, amesema ameridhishwa na maendeleo ya uzalishaji katika mgodi wa STAMIGOLD na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza ili kuimarisha ufanisi na mchango wake kiuchumi.
Akizungumza baada ya kukagua shughuli za uchimbaji katika mgodi huo uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera, Sirro alisema Bodi imejipanga kuusimamia kwa karibu mgodi huo kupitia Menejimenti ya STAMICO kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na mapato kwa taifa.
Alibainisha kuwa tangu kuanza kwa uzalishaji mwaka 2013, STAMIGOLD imepiga hatua kubwa katika kujitegemea kiutendaji, ikiwemo uwezo wa kugharamia shughuli zake muhimu kama manunuzi bila utegemezi wa moja kwa moja kutoka Hazina.
Aidha, aliielekeza Menejimenti kuimarisha tafiti za kijiolojia ili kubaini maeneo mapya yenye uwezekano wa uchimbaji, kupanua uwekezaji na kuongeza uhai wa mgodi huo kwa manufaa ya muda mrefu ya uchumi wa nchi. Sambamba na hilo, alisisitiza umuhimu wa nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa watendaji wote wanaosimamia shughuli za mgodi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Deusdedith Magala, alisema STAMIGOLD imeanza utekelezaji wa miradi mipya katika maeneo matatu ya uchimbaji yanayotarajiwa kuongeza kiwango cha uzalishaji kwa kiasi kikubwa.
“Ndani ya miezi minne ijayo, hadi kufikia Juni 2026, tunatarajia kuzalisha wakia 8,000 za dhahabu. Tunayo imani kuwa hatua hii itaongeza uthabiti wa kiuchumi wa mgodi na kuchangia zaidi mapato ya taifa,” alisema Magala.
Aliongeza kuwa kampuni imepanga kufanya tafiti katika leseni ambazo bado hazijaguswa ili kuongeza muda wa uhai wa mgodi kutoka makadirio ya miaka mitano iliyobaki hadi zaidi ya miaka 10.
Meneja Mkuu wa STAMIGOLD, Ali Said, alisema mgodi huo kwa sasa unaajiri wafanyakazi 613 wanaotekeleza majukumu yao kwa lengo la kuongeza tija na mapato ya uzalishaji.
Alibainisha kuwa tangu kuanza kwa uzalishaji mwaka 2013, STAMIGOLD imechangia takribani shilingi bilioni 56 kwa Serikali, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha uwekezaji huo unawanufaisha Watanzania moja kwa moja.
Aidha, aliihakikishia Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO kuwa utatuzi wa changamoto za kiutendaji unaendelea na unatarajiwa kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kilo 30 za dhahabu kwa mwezi hadi kiwango cha juu zaidi katika kipindi kijacho.
MWISHO






0 Comments