Na ArushaDigital – Dar es Salaam
Tume inayochunguza matukio ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imeendelea na zoezi la kukusanya ushahidi na maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwemo mahojiano na aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya.
Mahojiano hayo yamefanyika katika ofisi za Tume zilizopo ndani ya jengo la Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ambapo Sabaya alitoa maoni, tathmini na mapendekezo yake kuhusu chanzo, mwenendo na athari za matukio hayo kwa wananchi pamoja na miundombinu ya kijamii na kiuchumi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Tume, mazungumzo hayo yalijikita katika uchambuzi wa kina wa mazingira yaliyopelekea kuzuka kwa vurugu, namna zilivyoathiri usalama wa raia na mali zao, pamoja na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuimarisha utulivu wa kisiasa na kijamii nchini Tanzania.
Aidha, Tume imeeleza kuwa maoni na ushauri unaotolewa na viongozi wa sasa na wastaafu ni sehemu muhimu ya mchakato wa kuandaa mapendekezo ya sera na hatua za kiutawala zitakazosaidia kuzuia kujirudia kwa matukio ya uvunjifu wa amani katika chaguzi zijazo.
Uchunguzi huo unaendelea kwa kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa na kitaaluma ili kuhakikisha tathmini inayotolewa inawakilisha taswira halisi ya yaliyojiri na kuweka msingi wa maboresho ya kudumu katika mifumo ya usimamizi wa uchaguzi na ulinzi wa amani ya taifa.


0 Comments