MGODI WA MAREHEMU MATHIAS MANGA MERERANI WAFUNGIWA BAADA YA MFANYAKAZI KUFA KWA KUVUTA HEWA CHAFU, FAMILIA YAGEUKA BUBU!

 Na Joseph Ngilisho – MANYARA


Mgodi wa Manga–Manga Gems, unaomilikiwa na mfanyabiashara maarufu marehemu Mathias Manga, uliopo Kitalu D katika eneo la Mererani mkoani Manyara, umefungwa kwa muda usiojulikana kufuatia kifo cha mfanyakazi wake, Frank Joseph William (32), aliyefariki dunia baada ya kuvuta hewa chafu ndani ya mgodi huo, bila kuwepo kwa tahadhari stahiki za kiusalama.


Tukio hilo la kusikitisha linadaiwa kutokea Januari 31, 2026, wakati marehemu alipokwenda kujisaidia katika eneo la bomba lenye hewa chafu (toxic air shaft) ndani ya mgodi huo, hali iliyosababisha kukosa hewa ya oksijeni na hatimaye kupoteza maisha.


Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Afisa Mkazi wa Madini Mererani (RMO), George Kaseza, alisema kuwa mamlaka za madini zimechukua hatua ya kufunga mgodi huo mara moja ili kupisha uchunguzi wa kina kuhusu mazingira ya kazi na uzingatiaji wa sheria na kanuni za usalama migodini.


“Ni kweli tukio limetokea katika Mgodi wa Manga–Manga Gems. Marehemu alitoka kwenda kujisaidia katika bomba lenye hewa chafu, akakosa hewa na baadaye kupoteza maisha. Kwa sasa tumeufungia mgodi huo kupisha uchunguzi wa kina,” alisema Kaseza.


Hata hivyo, taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika eneo la tukio zinaeleza kuwa, baada ya kifo hicho, mwili wa marehemu ulisafirishwa kimya kimya kutoka Mererani na kupelekwa kuzikwa, bila kutolewa taarifa ya wazi kwa umma wala maelezo ya kina kuhusu taratibu zilizofuatwa kabla ya mazishi, hali iliyoibua maswali mapya kuhusu mwenendo wa tukio hilo.


Katika jitihada za kupata ufafanuzi zaidi, mwandishi wa habari hii alimtafuta mke wa marehemu Mathias Manga, Bi. Bakhita Manga, kwa njia ya simu ili kupata kauli yake kuhusiana na madai hayo. 


Akijibu maswali hayo,  Bakhita Manga alisema hahusiki na mgodi huo na kwamba hana taarifa zozote kuhusu tukio lililotokea, akisisitiza kuwa hajui chochote kinachohusiana na uendeshaji wa mgodi huo.


Kauli hiyo imeongeza mjadala mpana kuhusu umiliki, usimamizi na uwajibikaji wa migodi, hususan ile inayomilikiwa au kuhusishwa na warithi wa wafanyabiashara waliotangulia mbele ya haki.


Kwa upande wao, wachambuzi wa masuala ya ajira na usalama kazini wanasema kuwa kifo cha mfanyakazi katika mazingira ya mgodi kinapaswa kuhusisha uchunguzi wa wazi, uwazi wa taarifa, ushirikishwaji wa familia ya marehemu pamoja na taratibu za kisheria kabla ya mazishi, ili kuhakikisha haki na uwajibikaji vinazingatiwa kikamilifu.


Kifo cha Frank Joseph William kimeendelea kuibua hofu miongoni mwa wachimbaji wadogo na wafanyakazi wa migodi ya vito katika eneo la Mererani, huku wadau wa sekta ya madini wakiiomba serikali kuimarisha ukaguzi wa mara kwa mara, kusimamia matumizi ya vifaa vya kinga binafsi na kuhakikisha wamiliki wa migodi wanawajibika ipasavyo kwa usalama wa wafanyakazi wao.


Uchunguzi wa serikali kuhusu tukio hilo unaendelea, na mamlaka zimeonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kukiuka sheria au kusababisha uzembe uliosababisha kupotea kwa maisha ya mfanyakazi huyo.


Ends..

Post a Comment

0 Comments