FUTARI YA PAMOJA KARATU: MHESHIMIWA PARESSO AKABIDHI MISAADA KWA WAISLAMU
Na Joseph Ngilisho – KARATU
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha na Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Paresso, leo tarehe 27 Februari 2026 amefuturisha Waislamu katika Msikiti wa Karatu Mjini, wilayani Karatu.
Tukio hilo la kidini na kijamii lililofanyika wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani limebeba ujumbe wa kuimarisha mshikamano wa jamii, kukuza maadili mema na kuendeleza roho ya kusaidiana miongoni mwa waumini na wananchi kwa ujumla.
Katika hafla hiyo, Mheshimiwa Paresso amekabidhi msaada mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya ibada na kuwajengea vijana msingi imara wa maadili ya dini. Misaada iliyotolewa ni pamoja na,Juzuu 100 za Qur’ani,Misahafu 50,Tasbihi,Kanzu na Kofia (baraghashe)
Mbali na vifaa hivyo, Mheshimiwa Paresso amekabidhi pia mkono wa sadaka wa shilingi 1,000,000 kwa ajili ya kusaidia shughuli za msikiti na miradi ya kijamii inayogusa maisha ya waumini na wakazi wa Karatu kwa ujumla.
Akizungumza na waumini baada ya futari, Mheshimiwa Paresso amesisitiza umuhimu wa umoja, mshikamano na kudumisha maadili mema katika jamii, akibainisha kuwa maendeleo ya taifa hujengwa juu ya misingi ya hofu ya Mungu, upendo na ushirikiano wa wananchi.
Waumini na viongozi wa msikiti walimshukuru Mheshimiwa Paresso kwa mchango huo, wakieleza kuwa msaada uliotolewa utachangia kuimarisha ibada, malezi ya vijana na ustawi wa kijamii katika eneo hilo.
Tukio hilo limeakisi dhamira ya viongozi kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kidini, huku likiwa kichocheo cha kuendeleza mshikamano na amani katika jamii ya Tanzania.
Ends



0 Comments