MBUNGE GIDO AKOLEZA MOTO WA BARABARA ZA LAMI ARUSHA,AMWAMBIA WAZIRI MKUU JIJI LA ARUSHA LINAHITAJI KUNG'ARA KWA LAMI KABLA YA AFCON.

 MBUNGE MARIRTHA GIDO AOMBA BARABARA ZA LAMI ARUSHA KABLA YA AFCON

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Marirtha Gido, amemwomba Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, kuharakisha ujenzi na ukarabati wa barabara za lami katika Jiji la Arusha, akisisitiza kuwa maboresho hayo ni muhimu kabla ya ujio wa mashindano ya AFCON.

Gido alitoa ombi hilo wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Soko la Kilombero, akieleza kuwa Arusha ni kitovu cha utalii na biashara kinachotarajiwa kupokea wageni wengi wa kimataifa, hivyo kinapaswa kuwa na miundombinu ya kisasa na inayokidhi hadhi yake.

Alisema kuwa pamoja na juhudi za Serikali kuboresha huduma za jamii na miradi ya maendeleo, bado kuna changamoto ya baadhi ya barabara kuwa katika hali isiyoridhisha, hali inayosababisha msongamano wa magari, ucheleweshaji wa huduma za usafirishaji na kupunguza ufanisi wa shughuli za kiuchumi.

“Arusha ni lango la utalii wa Tanzania na sasa linajiandaa kupokea tukio kubwa la kimataifa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuharakisha ujenzi wa barabara za lami ili jiji letu liwe tayari kupokea wageni kwa hadhi inayostahili,” alisema Gido huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu alieleza kuwa Serikali inaendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya miji mikubwa nchini ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Alisisitiza kuwa maandalizi ya matukio ya kimataifa yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali Kuu, mamlaka za mitaa na wadau wa maendeleo.

Kauli ya mbunge huyo imeongeza hamasa kwa wakazi wa Arusha, wengi wao wakieleza matumaini kuwa maboresho ya barabara yatachochea biashara, kuongeza mvuto wa uwekezaji na kulifanya jiji hilo kuwa tayari kwa mapokezi ya wageni wa kimataifa katika mashindano yajayo ya AFCON.





Ends. 

Post a Comment

0 Comments