BARAZA LA MADIWANI NGORONGORO LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 45.2 KWA 2026/2027

 BARAZA LA MADIWANI NGORONGORO LAPITISHA BAJETI YA BILIONI 45.2 KWA 2026/2027

Na Joseph Ngilisho – NGORONGORO 

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ngorongoro limepitisha Bajeti ya Shilingi bilioni 45.2 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ikilenga kuimarisha huduma za kijamii, kukuza uchumi wa wananchi na kuongeza ufanisi wa utendaji wa Halmashauri.

Bajeti hiyo iliwasilishwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na Afisa Mipango, Emmy Hongoli, aliyebainisha kuwa fedha hizo zitatokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo mapato ya ndani Sh bilioni 4.1, mishahara ya watumishi Sh bilioni 22.7, michango ya wahisani Sh bilioni 4.4 na Serikali Kuu Sh bilioni 13.9.


Kwa upande wa matumizi, Halmashauri imepanga kutumia jumla ya Sh bilioni 45.2 ambapo Sh bilioni 4.1 zitatokana na mapato ya ndani, Sh bilioni 22.7 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi, huku Sh bilioni 18.9 zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.

Vipaumbele saba vya maendeleo

Bi. Hongoli alieleza kuwa bajeti hiyo imejikita katika vipaumbele saba muhimu: kuongeza mapato ya ndani kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji, kuboresha elimu, kuimarisha huduma za afya, kuboresha masilahi ya watumishi, kuinua sekta za kilimo na mifugo, kuimarisha uhifadhi na utalii pamoja na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10.

Akifungua mkutano wa Baraza hilo, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Manja Sironga Yaile, alisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na imegusa kata zote 28 za Halmashauri.

Alisisitiza wajibu wa madiwani kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao ili kuhakikisha utekelezaji wa bajeti unafanikiwa kama ulivyopangwa.

Usimamizi na ukusanyaji wa mapato waimarishwa

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Benezeth Bikizo, aliwashukuru madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo na kuahidi kuwa wataalamu wa Halmashauri wamejipanga kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Serikali.

Aliongeza kuwa ukusanyaji wa mapato ya ndani sasa unafanyika kwa kutumia mifumo ya kielektroniki na kuonya kuwa ni kosa kisheria kwa mkusanyaji kutoa risiti isiyotokana na mashine ya kielektroniki. Pia aliwataka madiwani kuhakikisha watendaji katika kata na vijiji wanatumia mashine rasmi za utoaji risiti ili kuongeza uwazi na ufanisi wa mapato ya Halmashauri.

Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatarajiwa kuimarisha utoaji wa huduma na kuchochea maendeleo endelevu kwa wananchi wa Ngorongoro katika mwaka wa fedha ujao.


ENDS..

Post a Comment

0 Comments