BALOZI DKT KUSILUKA AFUNGUA KIKAO CHA SITA SERIKALI MTANDAO eGA,ASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KUWAHUDUMIA WANANCHI

 Balozi Dkt Moses Kusiluka Afungua Kikao cha Sita cha Serikali Mtandao eGA Arusha

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA 

ARUSHA –Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt Moses Kusiluka, amefungua rasmi kikao kazi cha sita cha Serikali Mtandao (eGA) kinachofanyika kwa siku tatu katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC), Arusha, akisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza leo February 17,2026 na washiriki, Balozi Dkt Kusiluka alisema kuwa teknolojia ni chombo cha msingi cha kuhakikisha huduma za umma zinatolewa haraka, kwa uwazi, salama, rahisi na kwa gharama nafuu.

“Huduma za serikali zinapaswa kuwa bora na kupatikana kwa wakati unaofaa, na teknolojia ndiyo nyenzo inayoweza kutimiza hili,” alisema.

Kauli mbiu ya kikao ni “Huduma Bora za Umma Kupitia Teknolojia”, ikilenga malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Uchumi 2050, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya huduma za serikali zinatarajiwa kufanikishwa kidijitali.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Nomba, amesema serikali imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma za umma kupitia mifumo ya kidijitali.

 Mkutano wa siku tatu umewaleta pamoja washiriki 400 kutoka sekta za umma na binafsi kujadili maendeleo, changamoto na mustakabali wa huduma za kidijitali serikalini.

“eGA imeimarisha usimamizi wa miradi ya TEHAMA serikalini, kuendeleza mtandao wa mawasiliano ya serikali, na kusimamia vituo vya kitaifa vya kuhifadhi data vinavyowezesha taasisi za umma kuendesha mifumo yao kwa usalama,” alisema Nomba.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Toba Nguvila, amesema mkoa huo utaendelea kuwa kinara wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Alisema Arusha imekuwa mwenyeji wa mikutano ya kitaifa ya serikali kwa miaka sita mfululizo kutokana na miundombinu bora na utayari wa kuunga mkono mageuzi ya kidijitali.

“Serikali ya Mkoa wa Arusha itaendelea kutekeleza maelekezo ya kitaifa katika kuimarisha utawala wa kidijitali na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi,” alisema Nguvila.

Mkoa pia unaendelea na maandalizi ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa AFCON mwaka ujao, tukio litakalochochea ukuaji wa uchumi na uwekezaji wa utalii.

Zanzibar Yashirikiana Kuboresha Huduma za Kidijitali

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar (eGAZ), Said Seif, alisema ushirikiano kati ya serikali, taasisi za mawasiliano na wadau wa teknolojia unaendelea kuimarisha mageuzi ya kidijitali.

Mageuzi ya kidijitali si chaguo bali ni hitaji la msingi katika maendeleo ya taifa. Ushirikiano huu umewezesha usalama wa mifumo ya kidijitali, upatikanaji wa huduma za mtandao, na matumizi ya teknolojia bunifu kama IoT,” alisema Seif.


Seif alisisitiza kuwa uongozi na uratibu imara wa taasisi za serikali mtandao ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa.





Ends....

Post a Comment

0 Comments