WAFANYAKAZI ZAIDI YA 100 WA KIWANDA CHA COMFY ARUSHA WAGOMA KAZI, WALALAMIKIA MANYANYASO, MISHARA DUNI NA MAZINGIRA HATARISHI WAHOFIA MAAFA.
Na Joseph Ngilisho – ARUSHA
ZAIDI ya wafanyakazi 100 wa kiwanda cha Pan Africa Enterprises kinachozalisha magodoro ya Comfy, kilichopo Njiro jijini Arusha, wamegoma kazi wakilalamikia kile walichodai ni manyanyaso kazini, mapunjo ya mshahara, mazingira duni na hatarishi ya kazi pamoja na kukosa haki za msingi za ajira.Wafanyakazi hao, waliokusanyika jana mbele ya lango la kiwanda hicho, walisema wanalipwa mshahara wa shilingi 165,000 kabla ya makato ya kodi na michango mingine, kiasi wanachodai ni kinyume cha taratibu za kisheria na hakitoshelezi mahitaji ya msingi ya maisha.
Walidai wameendelea kulipwa kiwango hicho kwa zaidi ya miaka mitano bila mabadiliko yoyote licha ya kupanda kwa gharama za maisha.
Mbali na mshahara duni, wafanyakazi hao walieleza kufanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, wakidai kiwanda hicho hakina miundombinu rafiki ya hewa hali inayosababisha vumbi jingi na hatari ya kiafya. Waliongeza kuwa hali hiyo huibua hofu ya kutokea maafa wakati wowote wakiwa kazini.
“Hatuna mikataba ya ajira, hatupewi vitendea kazi muhimu kama maski, viatu vya kiwandani wala maziwa kwa ajili ya kukabiliana na vumbi la magodoro tunalofanya nalo kazi kila siku,” alisema Justine Julias mmoja wa wafanyakazi kwa niaba ya wenzake.
Wafanyakazi hao pia walimtuhumu mwajiri wao, waliyemtaja kwa jina la Patrick Shah, kwa kile walichodai ni kuwanyima haki mbalimbali ikiwemo mikopo ya bidhaa wanazozalisha wenyewe, kama magodoro, wakisema kipato chao hakiwaruhusu hata kujinunulia bidhaa hizo.
Aidha walidai mfumo wa malipo hauko wazi, wakisema mshahara wa msingi unachanganywa na malipo ya ziada ya muda wa ziada (overtime), hali inayowachanganya kutambua haki zao halisi.
“Mshahara ulikuwa shilingi 150,000, hadi sasa hatujaona mabadiliko yanayoeleweka. Tunataka mshahara utenganishwe na malipo ya overtime ili tujue haki zetu. Pia hatujui kima cha chini cha mshahara wa sekta ya viwanda ni kiasi gani kwa sasa,” alisema mfanyakazi mwingine Seleman Yusuphu
Katika madai yao, wafanyakazi hao walieleza kukosa uhuru kazini, wakisema hufanya kazi kwa vitisho vya kufukuzwa jambo linalowanyima amani.
Walidai pia kuwepo kwa upendeleo kazini, ambapo baadhi ya wafanyakazi hupewa bonasi mwishoni mwa mwezi huku wengine wakiachwa bila maelezo, pamoja na madai ya uongozi kuwa na mahusiano ya karibu na wafanyakazi wa kike hali wanayodai hupunguza nidhamu kazini.
Aidha walilalamikia kukosa ushirikiano kutoka kwa mwajiri pindi mfanyakazi anapopatwa na msiba.
Kutokana na hali hiyo, wafanyakazi hao waliitaka serikali kupitia wizara yenye dhamana ya kazi na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa viwanda kufanya ukaguzi wa kina katika kiwanda hicho ili kubaini ukweli wa madai yao na kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza baadaye.
Akijibu hoja hizo mbele ya viongozi wa Idara ya Kazi waliofika kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi, Mkurugenzi wa kiwanda hicho Patrick Shah alisema amepokea madai yote na kuyaahidi kuyafanyia kazi, ikiwemo suala la nyongeza ya mshahara kufikia shilingi 200,000 kama ilivyotangazwa na serikali kwa sekta ya viwanda.
Kwa upande wake, Goodluck Luginga, Afisa Kazi Mkoa wa Arusha, alifika katika kiwanda hicho na kutoa ufafanuzi kuhusu kima cha chini cha mshahara na taratibu za malipo kwa wafanyakazi wa viwandani.
Alisema serikali ilipotangaza nyongeza ya mishahara iliweka viwango maalum kwa kila sekta, ambapo katika sekta ya viwanda mshahara wa chini uliongezeka kutoka shilingi 150,000 hadi 200,000.
Alitoa wito kwa wafanyakazi kuacha migomo isiyo na tija na badala yake kufuata taratibu zilizopo ikiwemo majadiliano kati ya mwajiri, vyama vya wafanyakazi na Idara ya Kazi, akisema njia hiyo itasaidia kuondoa taharuki zisizo za lazima na kulinda haki za pande zote.
Baada ya ufafanuzi huo, Afisa Kazi aliwataka wafanyakazi kurejea kazini, ombi walilolitekeleza. Hata hivyo, wafanyakazi hao waliiomba Idara ya Kazi kufanya ukaguzi na ziara za mara kwa mara katika viwanda ili kufahamu changamoto zao na kutoa elimu pindi serikali inapofanya marekebisho ya mishahara na masharti ya ajira.
Mwisho.






0 Comments