Na Joseph Ngilisho – Arushadigital, Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, ambapo kiwango cha upatikanaji kimefikia takribani asilimia 90 ya mahitaji ya bidhaa hizo muhimu.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 21, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Johannes Lukumay, wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na Taasisi ya Utafiti wa Tiba (NIMR).
Dkt. Lukumay amesema juhudi zinazofanywa na taasisi hizo mbili zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wananchi. Hata hivyo, amebainisha kuwa pamoja na uwepo wa teknolojia za kisasa na vifaa tiba bora, bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa wananchi kuhusu matumizi na manufaa ya teknolojia hizo.
“Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, hususan kwenye dawa, vifaa tiba na teknolojia. Ni muhimu taasisi husika ziongeze juhudi za kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kuelewa na kunufaika ipasavyo na uwekezaji huu,” amesema Dkt. Lukumay.
Katika kikao hicho, Kamati pia imesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa dawa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Tiba (NIMR) katika kutafuta na kuendeleza vyanzo vya fedha kwa ajili ya uzalishaji, pamoja na kuongeza uwezo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika eneo la uzalishaji.
Hatua hiyo inalenga kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi na kuimarisha usalama wa afya ya Taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya kupitia MSD na NIMR, kwa lengo la kuboresha ubora wa huduma na kuhakikisha zinawafikia wananchi popote walipo.
Aidha, amesema katika kutekeleza maelekezo na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa maendeleo ya tiba asili. Kwa sasa, dawa za tiba asili zinapatikana katika hospitali 12 za rufaa za mikoa, hatua inayopanua wigo wa huduma za afya na kuwapa wananchi chaguo zaidi la huduma kulingana na mahitaji yao.
Ends..






0 Comments