MCHENGERWA ARIDHISHWA NA MABORESHO KITUO CHA AFYA KALOLENI, AAGIZA KIPANDISHWE HADHI KUWA HOSPITALI YA WILAYA,AAGIZA MGANGA MFAWIDHI KUPANDISHWA CHEO


MCHENGERWA ARIDHISHWA NA MABORESHO KITUO CHA AFYA KALOLENI, AAGIZA KIPANDISHWE HADHI KUWA HOSPITALI YA WILAYA

Na Joseph Ngilisho-– Arusha


WAZIRI wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ameridhishwa kwa kiwango kikubwa na maboresho pamoja na uwekezaji wa vifaa tiba vya kisasa uliofanywa katika Kituo cha Afya Kaloleni kilichopo jijini Arusha, akisema hatua hiyo imepanua kwa kiasi kikubwa wigo wa utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.


 Akizungumza leo Januari 26,2026 wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, Waziri Mchengerwa alisema kituo hicho kimepiga hatua kubwa za maendeleo, hasa kutokana na uwepo wa vifaa tiba vya kisasa vikiwemo mashine za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo mashine ya upimaji wa saratani ya matiti, jambo linalowawezesha wananchi kupata huduma za uchunguzi na matibabu kwa wakati bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kutokana na maendeleo hayo, Waziri Mchengerwa alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuanza mara moja mchakato wa kukipandisha hadhi Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya, ili kiweze kutoa huduma pana zaidi kulingana na mahitaji ya wakazi wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani.

Alisema ongezeko la idadi ya watu jijini Arusha pamoja na mahitaji yanayokua ya huduma za afya yanahitaji vituo vyenye uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi kwa ufanisi na kwa wakati.

Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa aliwapongeza viongozi wa Wilaya, Jiji la Arusha pamoja na menejimenti ya Kituo cha Afya Kaloleni kwa usimamizi mzuri, uwajibikaji na juhudi kubwa walizozionesha katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Kwa kutambua mchango wa kipekee wa uongozi katika kituo hicho, Waziri alimwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kuandaa Cheti Maalumu cha Pongezi kwa Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Kaloleni, Dkt. Anna Kimaro, kwa jitihada zake kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.

Aidha, Waziri aliagiza Dkt. Kimaro apandishwe cheo na kuzingatiwa kuwa Mganga Mfawidhi wa Wilaya kulingana na sifa na vyeti vyake vya kitaaluma (CV).

Cheti hicho kiliandaliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na kukabidhiwa rasmi na Waziri Mchengerwa katika hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa “Ongea na Waziri wa Afya”, uliofanyika leo katika Hospitali ya Rufaa ya Mt. Meru, jijini Arusha.

Hata hivyo, Waziri Mchengerwa alieleza kushangazwa na kusikitishwa na taarifa kuwa baadhi ya wagonjwa katika Kituo cha Afya Kaloleni wamekuwa wakielekezwa kununua dawa nje ya kituo hicho, jambo alilosema ni kinyume cha taratibu, maadili ya taaluma ya afya na haki za wagonjwa katika vituo vya umma.

Akitumia nafasi hiyo, Waziri alikemea vikali tabia hiyo na kuagiza ikomeshwe mara moja, akisisitiza kuwa ni marufuku kabisa kwa mgonjwa wa hospitali ya umma kutumwa kununua dawa nje ya kituo cha afya.

Zaidi ya hapo, aliwaagiza madaktari na wahusika wote wanaomiliki au kushirikiana na maduka ya famasia yaliyo jirani na hospitali kufunga biashara hizo mara moja, akionya kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.

Ziara ya Waziri Mchengerwa mkoani Arusha imeonesha kwa vitendo dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, dawa kwa wakati na kwa kuzingatia taratibu, huku ikidhibiti vitendo vinavyokiuka maadili ya taaluma ya afya na haki za wagonjwa.








Ends..

Post a Comment

0 Comments