Na Joseph Ngilisho – ARUMERU
MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumay, kwa kushirikiana na marafiki zake wanaoishi nchini Ujerumani, ametoa msaada wa nguo, vitabu pamoja na fedha taslimu kwa Kituo cha Malezi ya Watoto Yatima cha Jane Olevolos Orphans Center, kilichopo Kijiji cha Olevolos, Kata ya Kimnyaki, Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha.
Msaada huo umetolewa kufuatia safari ya kikazi ya Dkt. Lukumay nchini Ujerumani, ambako alikutana na marafiki zake walioguswa na changamoto zinazowakabili watoto yatima baada ya kutembelea kituo hicho mwaka jana.
Miongoni mwao ni rafiki yake mkubwa, Dkt. Ursula, raia wa Ujerumani, ambaye alifika kituoni hapo na kujionea hali halisi ya watoto wapatao 45 wanaolelewa katika kituo hicho.
Dkt. Lukumay alikabidhi msaada huo leo Januari 10, 2026, katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo, ambapo alisema msaada huo ni sehemu ya ahadi ya zawadi ya Krismasi iliyotolewa na marafiki zake wa Ujerumani baada ya kuguswa na mahitaji ya watoto hao.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Dkt. Lukumay alisema amekuwa akisaidia kituo hicho tangu mwaka 2019, hata kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge, na ameendelea kuwa karibu na watoto hao kama sehemu ya dhamira yake ya kusaidia makundi yenye uhitaji maalum.
“Nilipata nafasi ya kuwaleta marafiki zangu kutoka Ujerumani kutembelea kituo hiki mwaka jana. Waliguswa sana na changamoto walizoziona na wakaahidi kutoa msaada kama zawadi ya Krismasi kwa watoto hawa. Leo nimefurahi kutimiza ahadi hiyo kwa niaba yao,” alisema Dkt. Lukumay.
Aliongeza kuwa anajisikia fahari kubwa kushiriki katika malezi na ustawi wa watoto yatima, akiahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kituo hicho kinapata msaada endelevu.
Aidha, aliwashukuru marafiki zake wa Ujerumani kwa moyo wao wa upendo na kujitolea, akisema msaada huo umekuwa faraja kubwa kwa watoto na uongozi wa kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Jane Olevolos Orphans Center, Bi. Jane Mollel, alisema kituo hicho kilianzishwa mwaka 2005 kwa lengo la kutoa malezi, elimu na msaada wa kijamii kwa watoto yatima na wale walioko katika mazingira magumu.
Alisema tangu kuanzishwa kwake, kituo hicho kimesaidia jumla ya watoto 250 kupata elimu ya ngazi mbalimbali, kuanzia elimu ya awali hadi elimu ya juu, huku changamoto za mahitaji ya msingi na gharama za masomo zikiendelea kuwa kikwazo kikubwa.
“Tunamshukuru sana Dkt. Lukumay na marafiki zake kwa msaada huu mkubwa. Umekuwa faraja na matumaini mapya kwa watoto wetu,” alisema Bi. Mollel.
MWISHO









0 Comments