MBUNGE LUKUMAYE AAGIZA HUDUMA BORA OLTURUMENT, ATAKA UONGOZI UONDOKE VISINGIZIO

Na Joseph Ngilisho – ARUMERU


MBUNGE wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt. Johannes Lukumaye, ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Olturument na kuutaka uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila visingizio, akisisitiza kuwa dawa na vifaa tiba vinapatikana kwa takribani asilimia 90.

Akizungumza leo Januari 9,2026 wakati wa ziara hiyo, Dkt. Lukumay alieleza kuwa dhamira ya Serikali na uongozi wa hospitali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki, hususan wazee na akina mama wajawazito na wanaojifungua, bila kulazimika kuingia gharama zisizo za lazima.


Alikemea vikali malalamiko ya wananchi kuhusu akina mama wanaojifungua kulazimika kununua dawa na vifaa, akisema hali hiyo ni kinyume na mpango wa Serikali wa kutoa huduma za uzazi bure.


“Hakuna sababu ya akina mama wanaojifungua kuambiwa wanunue vifaa au dawa, wakati Serikali imeshatoa fedha na kuweka utaratibu wa huduma hizo kutolewa bila malipo,” alisema.


Mbunge huyo pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Arumeru Magharibi kwa kumuamini na kumchagua kuwa mbunge, akiahidi kuendelea kusimamia maslahi yao, hususan katika sekta ya afya.

 Aliutaka uongozi wa hospitali kushirikiana kwa karibu na viongozi wa vijiji na kata katika kusimamia maendeleo ya hospitali, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi hao kuwapa wananchi elimu kuhusu upatikanaji wa dawa, vipimo na huduma nyingine ili waache tabia ya kukimbilia hospitali za mbali pasipo sababu.


Aidha, Dkt. Lukumaye alipongeza hospitali hiyo kwa kupokea takribani shilingi bilioni 1.2 kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, fedha zilizotumika katika miradi mbalimbali ya maboresho ikiwemo ujenzi na ukarabati wa majengo ya hospitali.


Akizungumzia changamoto zilizoibuliwa wakati wa ziara hiyo, Mbunge huyo alitaja ukosefu wa uzio wa hospitali, barabara duni, ukosefu wa gari la usafiri, upatikanaji wa maji kwa zamu pamoja na upungufu wa watumishi, akiahidi kuzifanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Olturument, Dkt. Lootosim Zabron, alisema hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa rasilimali watu na miundombinu, hali inayokwamisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Wilaya ya Arumeru.


Alisema hospitali ina upungufu wa wauguzi 12 pamoja na uhaba wa wataalamu wawili wa mionzi, jambo linalosababisha mzigo mkubwa wa kazi kwa watumishi waliopo na kuchelewesha utoaji wa baadhi ya huduma.


“Uhaba huu unasababisha watumishi kufanya kazi kwa shinikizo kubwa, hali inayoweza kuathiri ubora wa huduma na ustawi wao,” alisema.


Dkt. Zabron aliongeza kuwa hospitali haina gari la usafiri kwa shughuli za kikazi, hali inayosababisha ugumu katika ufuatiliaji wa rufaa, usimamizi wa huduma na utekelezaji wa majukumu ya kitaalamu yanayohitaji usafiri wa uhakika.





Katika huduma za msingi, alisema hospitali inategemea maji ya mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (AUWSA) yanayopatikana kwa zamu, hali inayosababisha wakati mwingine huduma kusuasua, hususan katika maeneo nyeti kama maabara, vyumba vya upasuaji na wodi. Pia alitaja hali mbaya ya barabara zinazoelekea hospitalini kuwa kikwazo kikubwa kwa wagonjwa, hasa wanaohitaji huduma za dharura.


Changamoto nyingine aliyobainisha ni wizi wa vifaa vya hospitali, hususan mablanketi, unaofanywa na baadhi ya wagonjwa wanaolazwa, hali inayoongeza gharama za uendeshaji.


Hata hivyo, alimshukuru Mbunge Dkt. Lukumaye kwa kuendelea kuisemea hospitali hiyo na sekta ya afya kwa ujumla, pamoja na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha huduma za afya nchini.


Hospitali ya Wilaya ya Olturument inaendelea kutoa huduma kama Hospitali ya Wilaya (V.A), ambapo rufaa zote kutoka vituo vya afya na zahanati hupelekwa hapo.


Hospitali hiyo inahudumia wananchi wa Arumeru Magharibi na maeneo jirani, ikitoa huduma za upasuaji, maabara, kliniki ya baba, mama na mtoto (RCH), wagonjwa wa nje (OPD), wagonjwa wa ndani (IPD), uzazi na kujifungua, pamoja na huduma baada ya mimba kuharibika.


Huduma nyingine ni pamoja na uzazi wa mpango, huduma kwa wagonjwa wanaoishi na VVU, kifua kikuu na ukoma, magonjwa ya akili, huduma za macho, kinywa na meno, masikio, pua na koo (ENT), chumba cha kuhifadhia maiti, uchunguzi wa X-ray na Ultrasound, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, mazoezi ya viungo (Physiotherapy) na huduma za watoto wachanga wanaohitaji uangalizi maalum (NICU).


Hospitali pia inawahudumia makundi maalum yakiwemo wagonjwa wa dharura, wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, wazee kuanzia miaka 60 na wagonjwa wenye magonjwa sugu, pamoja na wagonjwa wanaotumia bima za afya zikiwemo NHIF na iCHF.





Ends...