KICHANGA CHATELEKEZWA GESTI NZEGA: DC ATANGAZA DONGE NONO LA SH. 500,000 KUMTAFUTA MAMA ALIYEJIFUNGUA NA BAADAYE KUTOKUWA NA MTOTO

By Arushadigital – NZEGA

Mwanamke mmoja ambaye utambulisho wake bado haujafahamika amejifungua mtoto mchanga na kumtelekeza katika nyumba ya kulala wageni (gesti) iliyopo Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, kabla ya kutoweka kusikojulikana, tukio lililozua mshtuko na huzuni katika jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwak Tukai, amesema amesikitishwa kwa kiasi kikubwa na kitendo hicho, akieleza kuwa ni kinyume na maadili ya jamii na ni ukatili wa hali ya juu dhidi ya mtoto mchanga. Aidha, ametangaza zawadi ya shilingi 500,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mama huyo.

Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa haiingii akilini kwa mama aliyeweza kubeba mimba kwa miezi tisa na kujifungua salama, kuamua kumtelekeza mtoto wake katika mazingira hatarishi. “Ni kitendo kisichokubalika kabisa. Mtoto huyu anastahili ulinzi, malezi na upendo wa mzazi wake,” alisema.

Alitoa wito kwa wananchi wenye taarifa zozote kuhusu mwanamke aliyekuwa mjamzito na sasa haonekani kuwa na mtoto, kujitokeza kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi au ofisini kwake, akiahidi kuwa taarifa hizo zitahifadhiwa kwa siri ili kumlinda mtoa taarifa.

Kwa mujibu wa DC Tukai, mtoto huyo anakadiriwa kuwa na umri wa takribani siku tatu tangu kuzaliwa, hali inayoashiria kuwa kumtelekeza kwake ni kumnyima haki zake za msingi ikiwemo kunyonya maziwa ya mama, kupata malezi stahiki na uangalizi wa karibu.

Akizungumzia tukio hilo, mhudumu wa gesti hiyo iliyopo Mtaa wa Ntinginya mjini Nzega, Christina Kahema, amesema mwanamke huyo alifika majira ya saa 1:30 jioni akiwa amejifunika kitenge na kubeba mtoto, kisha akaomba kupangiwa chumba.

Kahema aliongeza kuwa alipotoka kwa muda mfupi kumwonesha mteja mwingine chumba, aliporejea hakumkuta mwanamke huyo, bali alikuta mtoto mchanga amelazwa sakafuni eneo la mapokezi. Baada ya kubaini tukio hilo, walichukua hatua za haraka kumpeleka mtoto huyo katika Kituo cha Polisi.

Kwa upande wake, Daktari wa zamu wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dkt. Davis, amesema walimpokea mtoto huyo wa kike mwenye uzito wa kilo mbili na baada ya uchunguzi wa awali hawakubaini changamoto yoyote ya kiafya. Aliongeza kuwa mtoto huyo amepewa dawa za kuzuia maambukizi (antibiotiki) na kuanzishiwa lishe yenye virutubisho kulingana na umri wake, huku akiendelea kufuatiliwa na wataalamu wa afya.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku mamlaka za wilaya zikitoa wito kwa jamii kushirikiana ili kuhakikisha mama huyo anapatikana na haki za mtoto huyo zinalindwa kwa mujibu wa sheria.






Post a Comment

0 Comments