Simbu Azawadiwa Milioni 10 na TANAPA kwa Ushindi wa Dhahabu Dunia
Na Joseph Ngilisho, Arusha
Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limemzawadia mwanariadha nyota wa kimataifa, Alphonce Felix Simbu, kiasi cha shilingi milioni 10, kama pongezi kwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Dunia ya Riadha yaliyofanyika jijini Tokyo, Japan.
Hafla hiyo ilifanyika leo septembe 30,2025 katika makao makuu ya TANAPA jijini Arusha, ambapo Kamishna wa Uhifadhi, Juma Kuji, alisema ushindi huo wa Simbu si tu umeleta heshima kubwa kwa taifa, bali pia ni uthibitisho wa sera bora za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwekea mazingira mazuri michezo na utalii nchini.
“Huu ni ushindi wa taifa zima. TANAPA tunajivunia mafanikio ya Simbu kwani mbali na kuibua heshima kimataifa, ni fursa nyingine ya kutangaza vivutio vyetu vya utalii. Ushindi huu ni matunda ya juhudi za Rais Samia kupitia diplomasia ya michezo na filamu ya The Royal Tour,” alisema Kuji.
Kwa upande wake, Sajini Simbu alishukuru watanzania na serikali kwa mapokezi makubwa aliyopata, akiahidi kutetea taji hilo katika mashindano yajayo.
“Ninadeni kubwa kwa watanzania. Siri ya mafanikio haya ni nidhamu, kujituma na maandalizi makini. Nimejipanga kufanya vizuri zaidi ili kuendelea kulitangaza taifa,” alisema Simbu.
Aidha, alilishukuru Shirika la TANAPA kwa heshima ya kipekee ya kumpa kutumia gari maalum lililotumika na Rais Samia katika filamu ya The Royal Tour — ishara ya kuunganisha ushindi wake na utalii wa Tanzania.
Naye Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogart Steven, alisisitiza thamani kubwa ya medali hiyo akisema:
“Medali hii ya dhahabu ni ya kwanza kwa Tanzania na ina thamani ya zaidi ya dola elfu 70, sawa na shilingi milioni 700. Ni hatua kubwa katika historia ya michezo ya Tanzania.”
Kwa upande wake, Mohamed Hajji, Mkurugenzi wa Taasisi ya Twende Pamoja na Mama, taasisi iliyoteuliwa kuwa balozi wa utalii, alisema wamejipanga kumpeleka Simbu katika hifadhi mbalimbali ili kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania, wakimsapoti Rais Samia katika ajenda ya kukuza sekta hiyo.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa Simbu kupewa zawadi yake na kuahidiwa ushirikiano wa karibu na TANAPA na wadau wengine, katika safari yake ya michezo na utangazaji wa Tanzania kimataifa.
-Ends..
0 Comments