ARUSHA KUSIMAMA MAPOKEZI YA SAMIA,CCM YATAMBA KUWEKA REKODI YA AINA YAKE MIKOA MINGINE WATASUBIRI , WAJANE SOKO LA KILOMBERO WAMSHUKURU SAMIA WAAHIDI KUUJAZA UWANJA

 ARUSHA YASIMAMA: CCM KUPOKEA MGOMBEA URAIS KWA KISHINDO

Na Joseph Ngilisho – ARUSHA


KATIBU wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Saipulani Ramsey, amewataka wananchi wa Arusha kujiandaa kwa mapokezi makubwa ya mgombea urais wa CCM, akisema maandalizi yamepangwa kwa upekee wa aina yake.


Akizungumza na vyombo vya habari katika Soko Namba 68 la Kilombero, mbele ya akina mama wajasiriamali wadogo wa mboga mboga, Ramsey alisema tarehe 1 Oktoba 2025, mgombea huyo ataingia jijini Arusha na kusimama Usa River, Arumeru, ambapo atazungumza na wananchi.

Kwa mujibu wa Ramsey, siku inayofuata, tarehe 2 Oktoba 2025, mgombea huyo atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Mpira wa Sheikh Amri Abeid, ambapo wananchi wa Arusha wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi.

“Tutafanya mapokezi ya kishindo na tutawafundisha mikoa mingine namna gani mgombea urais anapokelewa. Tutaiweka rekodi sisi wenyewe na kuivunja sisi wenyewe. Hapa Arusha, mikoa mingine watasoma namba,” alisema Ramsey kwa msisitizo, akipigiwa makofi na akina mama wa soko hilo.

Katika hatua nyingine, Ramsey aliwaomba kina mama wa soko hilo kuunda vikundi ili waweze kunufaika na mikopo ya halmashauri, akisisitiza kuwa ni fursa ya kuinua mitaji yao na kukuza biashara ndogo ndogo. Aidha, alimwelekeza mgombea udiwani wa Kata ya Levolosi, lilipo soko hilo, kuhakikisha endapo atashinda nafasi hiyo, atasimamia ipasavyo mikopo hiyo ili akina mama wajasiriamali wanufaike kwa vitendo.

Aidha,  Salome Mollel maarufu Mama Mandonga mtu kazi, mmoja wa wamachinga wanaouza mboga katika soko hilo, alisema wanawake wa Arusha wako tayari kumpokea mgombea urais kwa furaha kubwa alimshukuru rais samia kwa kuwaona na kuwajengea Soko hilo ambapo kwa sasa wanaweza hata kujikimu kwa kipato ,nakuahidi kumuunga mkono.

“Tunamkaribisha kwa mikono miwili. Huu ni wakati wa wanawake na wananchi wote kuonyesha mshikamano wetu. Tutajitokeza kwa wingi na tutashiriki kikamilifu kumkaribisha kiongozi wetu,” alisema kwa tabasamu huku akishangiliwa na wenzake.

Ramsey aliongeza kuwa mapokezi hayo ni sehemu ya kuonyesha mshikamano wa wanaCCM na wananchi wa Arusha kwa mgombea wao, huku akiwataka wananchi wote kuungana kwa pamoja kuhakikisha historia mpya inaandikwa jijini humo.






Ends

Post a Comment

0 Comments