WAZIRI BITEKO AFUNGUA MAONESHO YA KARIBU-KILIFAIR ARUSHA,ATAKA YATUMIKE KUHAMASISHA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA UTALII,APONGEZA WAANDAAJI

Na Joseph Ngilisho-ARUSHA


NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa maonesho ya utalii ya Karibu– Kilifair yameendelea kukuwa kimataifa na kuwakutanisha wadau wa utalii kutoka maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili fursa za biashara, kubadilishana uzoefu katika biashara za utalii na masoko pamoja na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hiyo muhimu ya uchumi.


Dkt. Biteko amesema hayo leo Juni 6, 2025 jijini Arusha wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maonesho hayo ya kimataifa ya utalii ya Karibu -Kilifair 2025 yanayofanyika kuanzia Juni 5 hadi 8, 2025,jijini Arusha yenye kaulimbiu “Utalii Endelevu, Kujenga Ustahimilivu na Ubunifu”.


“Kwa mwaka huu pekee, maonesho haya yamekutanisha waoneshaji zaidi ya 500 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na zaidi ya nchi 10 duniani, wanunuzi wa kimataifa 1,000 kutoka zaidi ya mataifa 40 pamoja na maelfu ya wadau na wataalamu wa sekta ya utalii. Hii ni dhahiri kuwa, dunia inaiangalia Tanzania na Afrika Mashariki kuwa kitovu cha utalii. Tutumie fursa hii kutangaza vitu tulivyonavyo,” alisema Dkt. Biteko.


Alisema sekta ya utalii imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa maliasili na malikale, ustawi wa jamii na ukuaji wa kiuchumi. Ambapo takwimu zinaonesha kuwa, sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo ya nje.


Aliongeza kuwa Serikali inatekeleza programu mbalimbali za kimkakati za utangazaji utalii, zikiwemo filamu za Tanzania – the Royal Tour na Amazing Tanzania, ambazo zimeleta mafanikio makubwa kwa nchi. 





Kwa upande mwingine, Dkt. Biteko alisema Tanzania imeendelea kutambulika na kushinda tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo maarufu duniani za World Travel Awards – WTA zinazotolewa na Taasisi ya World Luxury Media Group Limited ya nchini Uingereza ambazo pia ni chachu katika kuvutia watalii katika soko la kimataifa.
















Tuzo hii ni matokeo ya Tanzania ya kutangaza ubora wa vivutio vilivyopo nchini kama vile Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mlima Kilimanjaro kuwa mahali bora pa kutembelea barani Afrika kwa shughuli za utalii wa safari na maeneo mbalimbali ikiwemo Zanzibar. Pia, Tanzania imepewa hadhi ya kuwa mwenyeji wa Tuzo za World Travel Awards kwa Kanda ya Afrika zitakazotolewa mwezi huu Juni, 2025,” amesema Dkt. Biteko.


Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kubuni njia mbalimbali za uendelezaji wa mazao ya utalii nchini kwa kuzingatia mgawanyiko wa aina ya mazao na mtawanyiko wa kijiografia wa nchi.


Maagizo mengine ni kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii badala ya kutangaza kwa kutumia majarida pekee na kushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali na Sekta binafsi katika kuboresha mazingira ya biashara za utalii nchini ili kuchochea na kuvutia uwekezaji zaidi.


Pia alitoa rai kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii hasa katika eneo la huduma za malazi, ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko kwa kuzingatia uwepo wa matukio mbalimbali ya kimataifa yanayoendelea kufanyika nchini.


Aidha, aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika nyanja mbalimbali ili kuhakikisha ustawi wa biashara za utalii nchini na maendeleo ya sekta kwa ujumla wake unanufaisha nchi. Sambamba na kuwataka Watanzania kuendelea kuwa wakarimu na kuelezea taswira nzuri ya nchi ili kuvutia wageni.


Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dustan Kitandula amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wenye maoni na kukuza sekta ya utalii nchini.


Akiongelea mafanikio ya sekta hiyo amesema inakuwa kwa kasi duniani hasa katika nchi mbalimbali mfano Tanzania ambapo mwaka 2024 imeingiza mapato ya utalii dola za marekani bilioni 3.9 pamoja na kupata watalii 5,360,247 ambapo watalii wa ndani ni 3,218,352 na watalii wa nje 2,218,352.


Katika kuendelea kuimarisha sekta hiyo nchini, alisema Serikali imeridhia kujenga ukumbi mkubwa wa kimataifa jijini Arusha kwa gharama ya shilingi bilioni 230. Aidha, Wizara yake imeendelea kushirikiana na wadau ili kukuza biashara kwa kuwa na vikao na wadau hao ambapo imefanya maboresho ya sheria ya ada na tozo kwa lengo la kukuza sekta hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya Karibu Kill Fair promotion  ,Dominic Shoo alisema onyesho hilo ni daraja la kikanda na ulimwengu katika kukuza utalii kutoka ndani na nje ya nchi. 


Alisema onyesho hilo limeshirikisha waonyeshaji zaidi ya 800  na wanunuzi zaidi ya 1000 ambao ni wanunuzi wa ndani na wa kimataifa kutoka nchi zaidi ya 40 pamoja na makampuni ya utalii zaidi ya 500 yameshiriki maonesho hayo


Aliiomba serikali  kuendelea kushirikiana na waandaaji wa onesho hilo ili lukuza utalii, ikiwemo kuvuta mawakala wa utalii wa ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha fursa za utalii zilizopo nchini zinakuwa kwa kasi


Mkuu wa Mkoa wa Arusha,Paul Makonda amewapongeza waandaji wa maonesho hayo ya Karibu – Kilifair na kusema kuwa ni kichocheo kikubwa cha uchumi mkoani humo, aidha amewaomba waandaji kuongeza idadi ya siku za maonesho kufikia siku tano hadi saba.

 Makonda, ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kulitambua eneo la Magereza - Kisongo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya kimataifa ya utalii ili kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali. Pia ameshauri muda wa maonesho hayo uongezwe kutoka siku 3 hadi siku 5 au 7 ili kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji kuonesha bidhaa na huduma zao, hasa zinazohusiana na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii


Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Andrea Murietha amesema kuwa Jumuiya hiyo imeendelea kufanya jitihada za kutangaza utalii kwa kufanya kazi karibu na nchi wanachama ili kuhakikisha manufaa ya utalii yanapatikama kwa usawa katika nchi hizo.


Ends....

Post a Comment

0 Comments