USHOGA ARUSHA UNATISHA WAWILI WAOLEWA KWA HARUSI UJERUMANI,DIWANI ATAKA ASILIMIA 10 YA MIKOPO YA HALMASHAURI WAPEWE VIJANA,CHAMATA KUWAKABILI WANAOMTUKANA RAIS MTANDAONI

 Na Joseph Ngilisho-ARUSHA

DIWANI wa Kata ya Sekei jijini Arusha,Gerald Sebastian amesema kuwa vijana wengi katika jiji hilo wamekengeuka na kujiingiza kwenye vitendo vya ushoga kiasi cha baadhi yao kuolewa nje ya nchi kwa harusi ,akitaka jitihada zaidi zifanyike kuwezesha vijana kupitia Mikopo ya halmashauri ili kuwanasua na janga hilo.


Akiongea leo juni 15,2025 jijini Arusha,kwa niaba ya meya wa jiji la Arusha pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha , katika maadhimisho ya siku ya wababa duniani iliyoandaliwa kimkoa na Taasisi ya Chanzo cha Matumaini Tanzania(CHAMATA),alisema kitendo vya mapenzi ya jinsia moja  iwapo kitafumbiwa macho kitaangamiza kizazi cha wanaume ambao ndio nguvu kazi ya taifa.


Alisema kuwa chanzo cha vijana kujiingiza kwenye vitendo hivyo ni kuporomoka kwa maadili yanayotokana na mifarakano ya wazazi huku baadhi ya wababa wakishindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa kuwaachia akinamama.


"Mimi nimeshuhudia vijana watatu wakazi wa jiji la Arusha,wakiolewa kwa harusi nchini ujerumani ,mmoja alikuwa akiishi Philips,Kimandolu na mwingine Sokon one na hawa ni baadhi tu wapo vijana wengi na hili ni janga linalotokana na mmomonyoko wa maadili"


Aliishauri serikali ili kupunguza  mifarakano ya kifamilia ambayo baadhi  inatokana na kipato duni, mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya akina mama  na makundi maalumu wapatiwe pia  kina baba kwa sababu baadhi ya akina mama wamekuwa wakiwanyanyasa waume zao kutokana na mitaji hiyo na hivyo kuibua mifarakano.


"Baba hutumia fedha zake nyingi kulea familia pamoja na kusomesha watoto na pindi anapozeeka huishiwa kipato na kuwa mpweke,mama na watoto huambatana na kumdharau baba yao na kama unavyojua heshima ya baba ni pamoja na kuwa na kipato "


Alisema hatua hiyo husababisha baba kushindwa kusimamia majukumu yake ya malezi badala yake watoto hujikuta wakijiingiza kwenye vitendo visivyofaa.


Awali mwenyekiti wa  Chanzo cha Matumaini Tanzania (CHAMATA)mch,Amani Silanga alisema maadhimisho ya siku ya wababa duniani hufanyika  juni 15 au 16 kila mwaka ikiwa lengo ni kuwakumbusha majukumu ya wababa pamoja na haki ya kuwaenzi wa baba ambao wamekuwa walezi wakuu wa familia.


Alisema historia ya siku ya Kina baba duniani(Father's Day) ilianzishwa Spokane Washington nchini Marekani  mwaka 1910  na Sonora Dodd mzaliwa wa Arkansas ambaye alilea watoto sita akiwa mzazi pekee , hivyo siku hiyo ikawa ni siku ya kuwaenzi kina baba wanaojitolea kuwalea watoto wao.



Mch,Silanga alisema chamata ni taasisi inayomuunga mkono rais Samia na chama cha Mapinduzi kwa kuhakikisha kinatangaza mema yaliyotekelezwa na serikali.


Aidha alisema Chamara  kimeshiriki maadhimisho ya siku ya wababa Duniani kwa kulaani kitendo cha matukio ya uhalifu  yanayoenezwa  mtandaoni kwa kumchafua Rais Samia Suluhu Hasani .


Alisema CHAMATA haipo   tayari kuona rais Samia akidhalilishwa mitandaoni na kukaa kimya bali wamejipanga kuwakabili wahalifu hao ambao wengi wao ni kutoka nchi Jirani.


"Lengo lingine la CHAMATA ni kuhakikisha wale wote wanaomchafua rais kwenye mitandao ya kijamii tunawajibu vilivyo kabla ya kujibiwa na mtu yoyote"


Alisema CHAMATA imeamua kutumia maadhimisho ya siku ya wababa duniani kutoa elimu dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya,unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.


Katika hatua nyingine CHAMATA imekabidhi vyeti vya pongezi kwa taasisi mbalimbali likiwemo jeshi la polisi mkoani Arusha, ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wao katika kulinda na kudumisha amani nchini.

Naye katibu wa Umoja wa wazee Mkoa wa Arusha(UWMA),Salim Mvungi alisema jukumu kubwa la umoja huo ni kuhakikisha wanailinda Amani ya nchi kwa kutoa elimu kwa jamii namma ya kujiepusha na maneno ya uchochezi.


Pia alisisitiza athari za utumiaji wa dawa za kulevya kwa vijana ambao wengi wao wamekuwa wakiathirika na matumizi ya  dawa za kulevya aina mpya aina ya Skanka .

"Jambo la kufanya kama mzazi ukifika nyumbani mkague mwanao katika begi lake mara kwa mara baadhi ya vijana wanatumia dawa za kulevya aina ya skanka"Alisema.













 

Ends......






Post a Comment

0 Comments