Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
KITUO cha Mafuta cha KGT kilichopo Dampo, kata ya Sokoni one Jijini Arusha,kinachomilikiwa na Mfanyabiashara Aloyce Mosha kimenusurika kuteketea kwa moto baada ya gari lililokuwa likishusha mafuta Kushika moto na kuwaka na kuzua taharuki kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na kituo hicho kujengwa eneo la makazi ya watu.
Majira ya mchana leo juni 11,2025, moto huo mkubwa ulitanda eneo la tukio ukiambatana na moshi mkubwa uliotanda angani wakati gari hilo la mafuta lenye nambaT 642 ABL aina ya Scania likishusha mafuta aina ya Petroli liliposhika moto kabla ya kudhibitiwa na kikosi cha zima moto saa moja baadaye.
Mamia ya wakazi wa eneo hilo walionekana wakikimbia ovyo na kutelekeza makazi yao wakihofia kulipukiwa na gari hilo lililokuwa likiwaka kwa kasi kubwa huku chanzo kikidaiwa ni gari hilo lenye teki la mafuta kushika moto wakati mafundi wa kuchomelea vyuma wakichomelea karibu na gari hilo .
Mmoja ya shuhuda wa tukio hilo,Ester Ruben alisema kuwa wakati anapita aliona watu wakichomelea vyuma katika eneo hilo la kituo cha mafuta lakini ghafla aliona gari limeshika moto na kuanza kuwaka kwa kasi kubwa na watu walianza kukimbia ovyo .
Naye diwani wa kata ya Sokoni one,Saluni Olodi alisema katika tukio hakuna madhara kwa binadamu ila alishauri mamlaka kuzingatia sheria na kuacha kutoa vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta kwenye makazi ya watu.
"Mimi siifundishi serikali namna ya kutekeleza majukumu yake ila ninachosema sheria zifuatwe ujenzi wa kituo cha mafuta kwenye makazi ya watu haikubaliki iwapo kama hili tenki linge pasuka madhara yangekuwa makubwa sana kwa binadamu ,ninachoshauri utaratibu wa kutoa vibali vya ujenzi wa vituo vya mafuta ufuatwe"Alisema Olodi
Mratibu Mwandamizi wa jeshi la zima moto Arusha,Osward Mwanjeware alisema mnamo majira ya saa 11.49 asubuhi walipokea taarifa za uwepo wa tukio la moto mkubwa katika kituo hicho cha mafuta.
"Askari wetu walifika kwa wakati na baada ya kuona moto ni mkubwa walilazimika kuagiza gari la pili na tulifanikisha kuzima moto huyo uliokuwa unawaka kwa kasi kubwa katika gari la mafuta na hakuna madhara kwa binadamu"
Osward alisema kuwa chanzo cha moto huo bado hakijajulikana ila unaonekana ulianzia mbali na wanaendelea na uchunguzi .Kuhusu kituo kujengwa kwenye makazi ya watu alisema kuwa vituo vya mafuta vinajengwa kwa mujibu wa sheria ila kama sheria haikufuatwa mamlaka zenyewe ndio zinapaswa kujibu.
Mmiliki wa Kituo hicho, Aloyce Mosha wala meneja wake hawakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo .
Ends...
0 Comments