Na Joseph Ngilisho-ARUSHA
SERIKALI kupitia Program ya Sequip imeendelea kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) kama suluhisho la changamoto ya upungufu wa walimu, kupitia mradi usambazaji wa vifaa vya Tehama kwa shule za sekondari nchini, wenye thamani ya Shilingi trilioni 1.2.
Akizungumzia katika hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya ugawaji wa vifaa vya TEHAMA (Smart blackboard)katika shule za sekondari nchini uliofanyika katika shule ya sekondari ya Arusha, Waziri Ofisi ya Rais – Tamisemi anayeshughulikia masuala ya elimu, Zainab Katimba, alisema mradi huo wa awamu ya pili unalenga kuzifikia shule 422 nchini.
Alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu inayolenga kuimarisha mazingira ya kujifunza kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini, kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa,ambapo teknolojia hiyo itarahisisha mwanafunzi kujifunza bila mwalimu kuwepo darasani.
Alisema kuwa vifaa hivyo vinavyozalishwa na kusambazwa na kampuni ya vifaa vya umeme ya TANZTECH,vitasaidia walimu kuongeza ufanisi katika ufundishaji na kuwapatia wanafunzi maarifa ya ziada, hasa katika maandalizi ya mitihani na ushiriki wao wa kujifunza katika muda wa ziada.
“Vifaa hivi vitasaidia pia kuandaa mazingira bora na ya kuvutia ya kujifunzia kwa wanafunzi, hasa wale wenye malengo ya kuwa wataalamu wa Tehama. Vilevile, vitaboresha stadi za kidijitali kwa walimu na wanafunzi, ikiwemo ufundishaji kwa vitendo,” amesema Katimba
Aidha, ametoa maelekezo kwa watendaji wa elimu ngazi zote kuhakikisha vifaa hivyo vinafikishwa kwa shule husika ndani ya siku tano, kutunzwa kwa matumizi ya muda mrefu, kulindwa, pamoja na kuwepo na mpango wa matengenezo endapo vitapata hitilafu. Alisisitiza pia umuhimu wa kuwa na walimu maalum wa kuratibu matumizi ya vifaa hivyo.
Katika hatua nyingine,Katimba amewataka walimu kufundisha kwa bidii kulingana na mabadiliko ya kisera ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa yanayohitajika katika karne ya sasa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema kuwa uzinduzi wa vifaa hivyo utasaidia kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya sayansi na kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inakuwa ya kiwango kinachofanana kote nchini. Aliwahimiza wanafunzi kutunza vifaa hivyo na kuwa na nidhamu ya matumizi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dkt. Selemani Shindika amesema vifaa hivyo vinavyogawiwa vinagarimu kiasi cha shilingi bilioni 12 na vitagawiwa kwa shule 422 za Sekondari ili kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa njia ya kisasa kwa kutumia TEHAMA ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Duniani.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Arusha, Lorna Christopher Ntelesi amesema kuwa changamoto ya upungufu wa walimu inakwenda kupungua kwa kiasi kikubwa kupitia matumizi ya Smartboard, ambapo wanafunzi wataweza kupata elimu bora hata pasipo kuwepo kwa walimu wa kutosha darasani.
Naye mwakilishi wa wanafunzi katika shule hiyo, Grace Tarimo, amesema kwa lugha ya Kiingereza: “Access of these modern tools in our school will further ensure that students have the ability to adapt to advanced environments in both academic and professional life.”.
Tafsiri.( “Upatikanaji wa vifaa hivi vya kisasa katika shule yetu utahakikisha zaidi kuwa wanafunzi wanakuwa na uwezo wa kuendana na mazingira ya kisasa katika maisha ya kitaaluma na maisha ya kazi.”)
Mradi huu wa Tehama unaendelea kutekelezwa katika Halmashauri zote nchini, ambapo awamu ya kwanza ilinufaisha shule 231 na awamu ya pili inayozinduliwa sasa inalenga kunufaisha shule 422 kote nchini.
0 Comments