Na Joseph Ngilisho- ARUSHA
HALMASHAURI ya Jiji la Arusha imefanya Makubaliano na kutiliana saini na mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya SUMA JKT Construction Company LTD kwa ajili ya ujenzi wa soko la Machinga kwa Morombo kwa Gharama ya sh,milioni 710,129,240.97.
Mradi mwingine uliosainiwa ni ujenzi wa uwanja wa michezo ambapo Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya STC Construction co Ltd alitunukiwa tuzo ya zabuni kwa gharama ya sh, bilioni 9,614,158,878,60.
Makubaliano hayo yamefanyika leo juni 17,2025, na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda pamoja na wananchi kwa wakandarasi wa kampuni hizo na jiji la Arusha ,kutiliana saini zabuni zenye thamani ya jumla ya sh, bilioni 10,324,288,119.57 yaliyofanyika katika eneo la mradi la Soko la Machinga kwa Morombo ,kata ya Muriet jijini hapa.
Akiongea mara baada ya kusaini kandarasi hiyo, Meneja wa Suma JKT Ujenzi kanda ya Kaskazini ,Luteni Kanali mhandisi Daud Zengo alisema kampuni yake inatekeleza mradi wa ujenzi wa soko na wanatarajia kukamilisha ndani ya muda uliopangwa wa miezi sita kama walivyokubaliana ili kupisha shughuli za uzalishaji ziweze kuendelea.
"Leo tumesaini kandarasi kwa ajili ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa soko la machinga baada ya kampuni yetu kushinda zabuni ambapo mkataba wetu ni miezi sita na tunatarajia kumaliza kazi hii kwa wakati na ikiwezekana tutamaliza kabla ya muda wa makubaliano"
Alisisitiza kufanyakazi kwa uadilifu kwa kuzingatia ubora unaotakiwa kwa kazi wanazopewa na serikali ili kujenga uaminifu kwa kampuni hiyo ya kizalendo iliyopo chini ya serikali .
Akisoma taarifa fupi ya miradi hiyo miwili kwa niaba ya Mkurugenzi wa jiji la Arusha ,John Kayombo, mganga Mkuu wa Halmashauri ya jiji la Arusha Dkt Maduhu Nindwa alisema kuwa miradi hiyo ni sehemu ya chanzo cha mapato ya halmashauri na itaongeza wigo wa kukusanya mapato ya halmashauri na hivyo kuchochea uchumi wa taifa.
Alisema soko hilo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya 80.
Kadharika mradi wa kiwanja cha mpira alisema ni maandalizi ya mashindano ya Afrika (AFCON)na utasaidia kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wa jiji la Arusha.
"Uwanja huo utajengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 9.6 na utakuwa na uwezo wa kubeba watazamaji 8,000 waliokaa. Pia utajumuisha viwanja vidogo vitatu vya mpira wa pete, mpira wa kikapu na tenisi na utatekelezwa na kampuni ya STC Construction Company Ltd na unalenga kuinua vipaji na kuongeza mapato kwa Jiji la Arusha".
Mkurugenzi wa jiji la Arusha John Kayombo alisema utekelezaji wa ujenzi wa kiwanja hicho cha michezo iwapo utakamilika jiji la Arusha litakuwa jiji la kwanza kuwa na ubunifu wa uwanja wake wa michezo katika halmashauri zote nchini.
Awali mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda alijivunia kuona utekelezaji wa miradi hiyo iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu ikisainiwa,licha ya kuwepo kwa mipango hiyo na fedha kutengwa tangu mwaka 2021.
Makonda alisisitiza kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika jiji la Arusha sio mipya bali ilikuwepo, akitolea mfano ujenzi wa soko la wamachinga alisema fedha zilitolewa na rais Samia Suluhu hasani kiasi cha sh,milioni 500 tangu mwaka 2021 lakini fedha zilikaa kwenye akaunti ya halmashauri ya jiji la Arusha bila kufanya kazi iliyokusudiwa kwa sababu ya mvutano wa viongozi.
"Nilipofika Arusha niligundua kuna fedha zimetolewa na rais Samia kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Machinga nilipowauliza kwa nini hawajengi hilo soko wakati fedha zipo,walisema kila wanapokaa na viongozi wa machinga na kukubaliana anaibuka mtu na kwenda kuwashawishi machinga wasikubali kujengewa soko eneo hilo"
Makonda alisema kuwa kuna kiongozi amekalia majungu na ushirikina kiasi kwamba alihusika kukwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Niliwaambia viongozi wa Jiji la Arusha, huu mwaka ukiisha soko halijajengwa, basi ama zao ama zangu. Leo nimefika hapa kushuhudia hatua hii muhimu mbele ya wananchi na tunataka miradi yote yenye fedha tayari itekelezwe kabla ya mwezi Julai ili wananchi waanze kunufaika,” amesisitiza Makonda.
Alisema tangu ameingia Arusha amefanikisha kusukuma miradi mbalimbali iliyokuwa imekwana ukiwemo mradi wa ujenzi wa Stendi ya mabasi eneo la Bon city ,Soko La Kilombero, Ukumbi wa Mikutano,Uwanja wa Michezo,Uwanja wa Mpira wa Afcon na ujenzi wa barabara za Lami ambayo kwa sasa anaona fahari miradi hiyo inatekelezwa kwa kasi kubwa na aliahidi hadi ifikapo julai 1mwaka huu hakutakuwa na mradi wowote ambao hautekelezwi.
Katika hatua nyingine Makonda amegawa pikipiki 23 pamoja na Bajaj mbili kwa watendaji wa kata zote za jiji la Arusha kwa ajili ya kuwarahisishia shughuli zao za kiutendaji kuwatumikia wananchi.
Makonda akifafanua kwamba fedha za kununua vyombo hivyo vya moto ni sehemu ya sh,milioni 300 zilizotengwa na halmashauri ya jiji hilo kwa ajili ya kununua gari la mstahiki meya .
"Nilimwomba mstahiki meya tubadilishe matumizi ya fedha hizo badala ya kununua gari la kifahari nilimshauri tununue vitendea kazi vya watendaji na fedha zilizobaki takribani milioni 180 nimeelekeza zijenge vivuko vya madaraja"Alisema
Naye meya wa jiji la Arusha Maxmilian Iranghe alisema kuwa katika kipindi cha Miezi sita halmashauri ya jiji la Arusha imeweza kusaini miradi ya zaidi ya bilioni 60 iliyotokana na jitihada kubwa za mkuu wa mkoa Makonda.
"Katika kipindi cha Miezi sita jiji la Arusha limefanikiwa kununua mitambo ya kutengeneza barabara,Mradi wa ujenzi wa stendi ya Bondeni city ,soko la kwa morombo ,Soko la Kilombero na eneo la mapumziko bustani ya Mto Themi"Alisema Meya.
Ends....
0 Comments