By arushadigtal -DODOMA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa ametangaza rasmi tarehe ya kuvunjwa kwa Mabaraza ya Madiwani katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa nchini, ikiwa ni hatua ya maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akitoa Tamko hilo leo Juni 15,2025 hapa Jjini Dodoma, Waziri Mchengerwa amesema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288, kifungu cha 84A, na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 178A, amesaini notisi mbili muhimu za kuvunjwa kwa Mabaraza hayo.
Amesema kwa mantiki hiyo vikao vya Halmashauri na kamati zake zinapaswa kuwa zimekoma ifikapo Juni 20,2025 na kuongeza kuwa kufanya kikao chochote cha Halmashauri au kamati yake baada ya tarehe hiyo itakuwa ni kukiuka notisi hizo.
“Kufanya kitendo hicho mtendaji mkuu wa Halmashauri ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri atapaswa kuwajibika, kwakuwa Mhe. Rais anatarajiwa kulivunja Bunge Juni 27,2025 mabaraza yote ya madiwani yanapaswa kuvunjwa rasmi ifikapo Juni 20,2025,”amesema.
Sambamba na hayo Mchengerwa amesema maelekezo ya kisheria na utaratibu baada ya kuvunjwa kwa mabaraza ni pamoja na kamati zote za Halmashauri zinasitishwa rasmi kuanzia Juni 20,2025 hadi pale uchaguzi mpya wa madiwani utakapofanyika.
“Lakini pia masuala yote ya kiutendaji katika Halmashauri yatasimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kipindi cha mpito akisaidiana na wakuu wa idara kama wajumbe wa kamati,”amesema.
Ameongeza kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hatoruhusiwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuanzisha miradi au uwekezaji mpya, kubadilisha au kurekebisha miradi, uwekezaji au uwamuzi wowote uliopitishwa na Halmashauri kabla ya kuvunjwa.
“Kutokutekeleza kwa ufanisi majukumu ya utawala kwa mujibu wa notisi hizi kutamfanya Mkurugenzi kuwajibika binafsi kwa mujibu wa sheria lakini pia Mkurugenzi wa Halmashauri atawasilisha taarifa ya maamuzi na mwenendo wa vikao vya Menejimenti vilivyofanyika wakati wa kipindi cha mpito katika kikao cha kwanza cha Baraza jipya la madiwani baada ya uchaguzi,”ameongeza.
Aidha Waziri huyo ametoa wito kwa wananchi, viongozi wa Serikali na wetandaji wote wa Halmashauri kushiriki kikamilifu katika kipindi hicho cha mpito kwa kuzingatia utawala bora, maadili ya utumishi wa umma na kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
“Nichukue fursa hii kama Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, nitoe pongezi na shukrani za dhati kwa Waheshimiwa madiwani wote nchini wanaokwenda kumaliza muda wao wa uongozi ifikapo Juni 20, 2025 nawapongeza kwa mchango wao mkubwa na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo yao, “amesema.
0 Comments